Mhubiri muuaji apewa hukumu kali - Kitale

Charles Nyachwara in court
Charles Nyachwara in court
Mhubiri mmoja amehukumiwa maiak 25 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi, kumpachika mimba na kisha kumuua kinyama msichana wa shule katika eneo la Kitale.

Charles Nyachwara, aliyekuwa mhubiri katika kainisa la Pentecostal Assemblies of God, alimuua mwanafunzi wa kidato cha nne aliyekuwa mjamzito, mwezi Julai mwaka 2011.

Jaji Hillary Chemitai alisema kwamba ushahidi uliyowasilishwa mahakamani ulidhihirisha kuwa mhubiri huyo alimuua mschana huyo kwa lengo la kuficha maovu yake.

“Nimesikiza pande zote, upande wa mashtaka na ule wa mshtakiwa. Ni wazi kuwa ulimtesa na kumuua msichana huyo. Uko huru kuasilisha rufaa,” Jaji alisema.

Nyachwara ambaye alikuwa pasta wa kanisa la Yuya PAG Cherengani alimuua Scolastica Mbihi, mwanafunzi wa shule ya upili ya Yuya, akiwa na mimba ya miezi mitano baada ya kuwa katika uhusiano naye kwa mwaka mmoja.

Msichana huyo alikuwa mwalimu wa ibada ya watoto katika kanisa ambalo Nyachwara alikuwa akiongoza.

Mahakama iliambiwa kuwa msichana huyo alikuwa tayari ameeleza wazazi wake kwamba alikuwa ametungwa mimba na mhubiri huyo.

Kisa hicho kiliripotiwa kwa polisi waliomkamata pasta huyo na kumfikisha katika mahakama ya Kitale ambako alifunguliwa mashtaka ya kunajisi. Aliachiliwa kwa dhamana.

Siku ya kuuawa, msichana huyo alikuwa anarejea nyumbani kutoka kliniki alipokutana na mhubiri huyo katika eneo la Kibomet.

Baada ya mazungumza mhubiri huyo alimshambulia Scholastica na kumdunga kisu mara kadhaa. Nyachwara kisha alitorokea katika shamba la mahindi kabla ya kukamatwa na mlinzi mmoja.

Ripoti ya upasuaji wa mwili wa Scholastica ilionyesha kwamba alikuwa na mimba ya watoto watatu.

Mhubiri huyo alifanyiwa uchunguzi wa kiakili na kuidhinishwa kujibu mashtaka ya mauaji.

Jamaa wake aliwasilisha dhamana ya shilingi milioni moja na akaachiliwa.

Baada ya kuachiliwa kwa dhamana alitoroka na kwenda mafichoni. Mkono wa sheria ni mrefu kwani alipatikana baada ya miaka mitano akiwa amejificha katika Wilaya ya Mbale, nchini Uganda, ambapo alikuwa amepata uraia wa nchi hiyo na hata kufungua kanisa lingine.

Alikuwa anajiandaa kufunga ndoa na mpenzi wake raia wa Uganda alipokamatwa na polisi na kurejeshwa nchini Kenya. Alikiri kuua Scolastica ili kuficha ukweli na kuokoa hadhi ya jina lake baada ya jaribio lake kutatua jambo hilo kuambulia patupu.