Mwanafunzi wa chuo kikuu aliyejaribu kuingia ikulu akiwa amejihami kwa kisu Brian Kibet amemwomba radhi rais Uhuru Kenyatta baada ya kufikishwa katika mahakama moja hapa jijini hivi leo . mashtaka dhidi yake hayakusomwa kwa sababu ripoti ya hali yake ya kiakili iliyofanywa na hospitali ya mathari imeonyesha kwamba ana ugonjwa unaotatizwa akili wa Schizophrenia. Ugonjwa huo huathiri uwezo wa kufikiria,matatizo ya kusema na pia kuvuruga mtu kujifahamu .Kibet alijipata matatani juni tarehe 10 mwaka huu alipojaribu kukwea ua la ikulu ya Nairobi akiwa amejihami kwa kisu .
Polisi waliokuwa wakilinda eneo hilo walimpiga risasi na begani na kumjeruhi na baadaye akapelekwa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta kwa matibabu .Kibet ni mwanafunzi wa mwaka wa tano wa uhandisi katika chuo kikuu cha JKUAT. Familia yake imetoa ombi kwa mahakama kuwaruhusu polisi kumhamisha hadi katika hospitali ya rufaa ya moi huko eldoret ambako aliwahi kutibiwa .
Korti itatoa uamuzi kuhusu ombi hilo la familia yake siku ya alhamisi lakini polisi wanataka kumzuilia katika hospitali ya Mathari hadi atakapokuwa katika hali nzuri ya kujibu mashtaka dhidi yake .