Wabunge wa Tangatanga wafurika mahakamani, kumuunga Itumbi mkono

Wabunge wa mrengo wa Tangatanga walimimika katika mahakama ya Milimani siku ya Alhamis kumuunga mkono Dennis Itumbi.

Itumbi alikamatwa na maafisa wa DCI siku ya Jumatano mjini Nairobi kuhusiana na barua feki iliyodai kuwepo kwa njama ya kumuua naibu rais William Ruto.  Wabunge waliofika mahakamani walijumuisha mbunge wa Kapseret Oscar Sudi, Didmus Baraza wa Kimilili, Kimani Ichungwa na mbunge wa Soy Caleb Kositany.

Upande wa mashtaka siku ya Alhamisi ulitaka Itumbi azuiliwe kwa siku 14 zaidi ili kuweza kukamilisha uchunguzi kuhusiano na madai dhidi yake. Kulingana na upande wa mashtaka, swala linalochunguzwa linaguzia usalama wa kitaifa na kwa hivyo kumwachilia kutafanya swala hilo kuonekana mzaha.

Upande wa mashtaka unataka simu yake ufanyiwe ukaguzi wa kina. Uchunguzi huo utajumuisha kukagua kikundi cha WhatsApp kwa jina Tangatanga Movement kilicho na wanachama 256.

Mawakili wa Itumbi walisema kwamba kukamatwa kwake ni viroja tu kwa sababu kundi wanalosema la Tangatanga lina wanachama 256 na ambao wote bado hawajakamatwa.