7 wamezea mate kiti cha Marehemu Ken Okoth

IMRAN
IMRAN
Siku chache baada ya mwili wa aliyekuwa mbunge wa Kibra Ken Okoth kuchomwa harakati za kurithi kiti chake zimeanza.

Wagombeaji saba tarayi wanaonekana kujibwaga uwanjani kutwaa wadhifa wa Okoth aliyefariki kutokana na maradhi ya saratani ya utumbo mwezi uliopita. Kakake mdogo Imran Okoth anaongoza orodha ya wanaopigiwa upatu kutwaa wadhifa huo.

Wengine ni aliyekuwa msaidizi wa Raila Eliud Owallo ambaye alibwagwa na Okoth katika uteuzi wa ODM kwenye uchaguzi wa mwaka 2017 na Ketta Onyango aliyekuwa msimamizi wa hazina ya CDF wakati Raila alikuwa mbunge wa Lang’ata pamoja na aliyekuwa Mwakilishi wa wadi ya Sarang’ombe Pius K’Otieno.

Palikuwepo fununu kwamba aliyekuwa mbunge wa Kasarani Elizabeth Ongoro, mwanasiasa mtajika katika kaunti ya Nairobi, alikuwa pia anamezea mate kiti hicho pamoja na Irshad Sumra aliyeshindwa katika uchaguzi mdogo wa Embakasi South mapema mwaka huu.

Marehemu Ken Okoth

Mshindi wa tuzo ya kimataifa kuhusu haki za binadamu Kennedy Odede pia anasemekana kukikodolea macho kiti hicho na kuna wengine wanaosema kwamba huenda katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna pia akajitosa uwanjani kutafuta kiti hicho. Familia ya marehemu Ken Okoth kwa kauli moja imeamua kumuunga mkono Imran, na kupiga jeki uwezo wake kumshawishi Raila kumuunga mkono huku akilenga kuendeleza kazi na mipango ya kakake, Okoth.

Mwenyekiti wa kitaifa wa ODM John Mbadi akizungumza na Gazeti la The Star kwa njia ya simu alisema kwamba idara husika ya chama hicho itajadili ombi la familia ya Okoth na kutoa uamuzi kama kitapeana tiketi ya moja kwa moja au kuruhusu wagombeaji wote kumenyana katika mchujo.

“Huo ni uamuzi ambao chama kitachukuwa wakati ufaao. Baraza la kitaifa ndilo lenye uwezo kutoa uamuzi. Nitaongoza mkutano wa baraza hilo wakati ufaao kujadili swala hilo na kutoa muongozo kuhusu swala hilo,” mbunge huyo wa Suba South alisema

Akizungumza na gazeti la The Star, binamuye Okoth, Elvis Oluoch alithibitisha kwamba wanapanga kutuma wawakilishi wa familia kwa kinara wa ODM na uongozi wa chama hicho ili wamuunge mkono jamaa wa familia ya Okoth ili kiti hicho kisaliye katika familia hiyo.