Mjumbe wako yupo? Wabunge wanaokosa vikao vya kamati wamulikwa

Duale anasema kwamba wabunge wengi hukosa kuhudhuria vikao vyao vya kamati bungeni lakini wanaponyimwa fursa za kwenda ziara za nje wanatishia kuwatoa mamlakani wakuu wao.

Kiongozi mkuu wa walio wengi bungeni Adan Duale anatarajiwa kutoa ripoti ya mahudhurio ya wabunge.

Wakati wa mjadala mkali, Duale alimweleza Spika Justin Muturi kuwa wakuu  wa kamati wameandaa orodha ya wanachama ambao wamekosa kuhudhuria kamati kwa zaidi ya mara tatu.

Amesema inasikitisha kuwa  hata baadhi ya wakuu wa makamati na manaibu wanakosa mikutano bila maelezo rasmi.

Anasema kwamba wakuu hao wa kamati wanakosa kuhudhuria mikutano kama njia ya kuhepa kujibu masuala muhimu yanayozingira kamati yao bungeni.

"Spika, wakuu wa kamati hii huhepa  mikutano, Tazama kamati ya Kilimo na Kamati ya Afya. Hakuna mbunge hapa kujibu maswali, "alisema.

Kamati ya Kilimo inaongozwa na Benjamin Washiali ilhali kamati ya Afya ikiongozwa na Sabina Chege.

Duale alisema kwa mujibu wa Maagizo ya Kudumu Bungeni, lazima mwanakamati awasilishe ombi lake la kutohudhruia kwa karani.

"Spika, nitaorodhesha ripoti iliyoandikwa na wakuu wa kamati kuhusu wanakamati ambao wamehudhuria, waliokosa kuhudhuria, pamoja na mikutano yote ambayo imehudhuriwa.'' alisema.

Sheria za bunge zinahitaji mwenye kiti na mwanachama wa kila kamati kuhudhuria vikao hadi saa 5 jioni.

Mbunge huyu wa mji wa Garissa alisema baadhi ya Wabunge hutia saini katika Bunge na kutoweka bila kuhudhuria vikao.

Duale aliwasuta baadhi ya wabunge hususan wa kamati za bunge ambao hukosa kuhudhuria vikao vyao na kutishia wanaponyimwa fursa ya kwenda katika ziara za nje.

'Kunao wale watakaongoza katika kutia sahihi ya kutokuwa na imani na wakuu wao wakinyimwa fursa ya kwenda ziara ilhali wanakosa kuhudhuria mikutano ya wanakamati,' alisema.

Aidha maoni ya Duale yaliungwa mkono na Spika Muturi ambaye alisema wanachama wote ambao wamekosa vikao kwa zaidi ya mara tatu watatupwa nje ya kamati.

"Tunataka kuona ripoti ya wanachama kuhudhuruia. Na iwapo siyuko mkutanoni, lazima naibu wangu ajuzwe. Iwapo hatutahudhuria vikao basi hauna maana katika taifa hili,' Spika Muturi alisema.