Nani mkali? KOT vs DCI. Jeshi la mtandao ambalo linafaa kuwajibika

Kenyans on Twitter au kwa  ufupi KOT, ni jeshi ambalo halina bunduki lakini athari za mashambulizi yake kutumia  maneno, vijembe, matusi, kejeli, picha na utani usiothibitiwa yanaweza  kusababisha  hata mtu kutamani kujiua .

Makali ya KOT yamewashangaza hata watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii na ingawaje  wengi huchukulia baadhi ya yanayochapishwa katika KOT kama burudani au mzaha, mengine sio mazuri yanayofaa kusifiwa kwa sababu yanawaathiri watu ambao wana hisia na  wanaokwaza zaidi ya mara moja na mambo yanayoandikwa katika mitandao .

Hata hivyo, baadhi ya vinavyochapishwa na KOT vinazua maswali ya je, mambo hayo hupatikanaje? Unafaa kuwa muangalifu kuhusu maisha yako na unaowaambia kuhusu kila hatua yako kwa sababu  KOT sio Aliens   ni watu kama mimi na wewe walio na  muda wa kutosha, bundles za kuharibu na  makovu yasiojulikana na hivyo basi  mtandao unawapa fursa bora ya kujiona wapo juu yako kwa kuyageuza maisha yako juu chini . Inakuaje  baadhi ya  vitu vya siri kabisa, vya ndani wakati mwingine vinapatikana mitandaoni? Ni kwa sababu baadhi ya watu unaowaamini wana akaunti feki za  kumbi za kijamii na wanazitumia kutoa siri kama hizo ama wanasambaza  siri zako ambazo badala yake hulipa jeshi  kama KOT  mambo ya kutosha kulipua kila unachopenda maishani mwako .

Nguvu na  ustadi wa jeshi la KOT zinafaa kutumiwa vizuri  kupigania masuala yanayowaathiri wakenya na kuwafanya viongozi wa kisiasa  na taasisi za umma kuwajibika . KOT inafaa kuanza kutumia uwezo wake kuleta machoni na katika mijadala masuala kama jinsi kodi yetu inavyotumiwa vibaya na ingawaje baadhi ya mambo ambayo wameweza kuyashughulikia hapo awali yanaweza kusifika kwa kuwashambulia watu waliostahili hasa wachokozi wenzao katika mataifa mengine kama vile vita vya mitandao vya mara kwa mara dhidi ya Nigeria, Uganda , Tanzania na hata Afrika Kusini. KOT  inafaa kuepuka kuingiza masuala ya kibinafsi ya watu hasa  walio mashuhuri kwa sababu vitu kama hivyo havijengi  ila vinabomoa .

Macelebs na  watu wengine wa kawaida ambao hushambuliwa na KOT  ni watu kama mimi na wewe na baadhi ya ukatili ambao huelekezewa haufai kabisa. KOT inafaa kutafuta mbinu za kutumia raslimali zilizopo kama uwepo wa mtandao na uhuru wa kutumia kumbi hizo kwa mambo yanayoleta manufaa ya jumla kwa wote bali sio  mambo kama kuwashambulia, kuwatusi na kuwafanyia kejeli watu kwa  sababu ya madai ya kusema hivi au kufanya vile . Kwa mfano mwanahabari Yvonne Okwara amejipata akipondwa sana na KOT kwa sababu ya msimamo wake kuhusu hatua ya baadhi ya watumizi wa mitandao kusambaza picha za utupu za  Brenda Cherotich ambaye alipona virusi vya Corona. Yvyonne alikuwa na haki ya kutoa maoni yake bila kuhofia adhabu ya kupigwa vijembe na kuchomwa wazi  katika grili ya KOT .

Utumiaji mbaya wa fursa za kuwepo uhuru na uwazi katika matumizi ya mitandao ndiko kunazozifanya baadhi ya serikali kubana matumzi ya mitandao miongoni mwa wananchi wao , na  tusije tukailazimu serikali zetu Afrika kuanza kubana  utumizi na uhuru wa mitandao kwa ajili ya   ukosefu wa kutowajibika kwa baadhi yetu na hasa jeshi lisilo na sura kama vile KOT .