Vifo vya nyumbani vya waathiriwa wa corona vyazua hofu huku mmoja akifariki mtaani Eastleigh

Kenya sasa imeanza kusajili vifo vya wagonjwa wa virusi vya corona wanaofariki wakiwa nyumbani. Mkurugenzi wa Afya nchini Patrick Amoth amesema hali hii inazua hofu kubwa kwamba watu wengi sasa wanaambukizwa virusi hivi katika jamiii.

Anasema vifo vya watu wawili katika kaunti ya Mombasa siku ya Jumatano vilitokea wakiwa nyumbani kwao. Anasema tishio kubwa sasa ni kwa wale watu ambao walikuwa wakiwauguza jamaa hao waliofariki.

“Wale wanaowashughulikia wagonjwa wa coronavirus wanakabiliwa na hatari ya juu zaidi kuambukizwa virusi hivyo. Hakikisha kwamba ukihisi mgonjwa piga simu kwa nambari ya simu 719 haraka,” Amoth Alisema.

Soma pia;

Anasema kwamba mtu mmoja aliyefariki katika kaunti ya Nairobi ambaye alikuwa miongoni mwa orodha ya wale waliotangazwa kufariki na katibu msimamizi katika wizara ya Afya Rashid Aman alikuwa kutoka mtaa wa Eastleigh na alifariki akiwa nyumbani kwake.

Amoth anasema hali hii inamaaminsha jamaa zake na hata majirani huenda tayari wameambukizwa maradhi haya. Mkurugenz huyo wa afaya aliongeza kuwa vifo vya corona vinavyotokea nyumbani ni ishara tosha kuwa virusi hivi sasa vimekita kambi katika jamii.

Amoth hata hivyo amasema idadi kubwa ya watu waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya corona nchini wako katika hali nzuri na kwamba mtu mmoja aliyekuwa katika mashine ya kumsaidia kupumua tayari ameondolewa kwa mashine hiyo na hali yake imeimarika.

Wizara ya Afya imesema kwamba watu wanne bado wanaendelea kutumia mashine za kupumua lakini hali zao zimeimarika na wataanza kutolewa pole pole. Kulingana na wizara ya Afya wengi walioambukizwa na virusi vya corona nchini Kenya hawajaonyesha dalili za ugonjwa huo ila tu dalili nyepesi.

Maambukizi ya virusi vya corona nchini Kenya sasa yamepita 600 baada ya watu 25 zaidi kuthibitishwa kuambukizwa virusi hivyo siku ya Alhamis. Jumla ya watu 29 wamefariki kutokana na virusi hivyo nchini ingawa wengi wao walikuwa pia na matatizo mengine ya kiafya.