Moto kama pasi! Sauti Sol wazindua kibao kipya 'Insecure' kwa ushirikiano na Radio Africa

Sauti Sol wakishirikiana na Radio Africa mapema leo  (Ijumaa) walizindua kibao kipya 'Insecure' moto kutoka jikoni.

Mastaa hao ambao kibao chao 'Suzanna' kinaendelea kutesa mawimbi katika mitandao ya kijamii wameshirikiana na kampuni ya Radio Africa kuzindua wimbo huu mpya huku wakijiandaa kuzindua albamu kali 'Midnight Train' mnamo Juni 5, mwaka huu.

Kibao hicho 'Insecure' kilizinduliwa kwa mpigo na kutesa mawimbi majira ya Ijumaa asubuhi katika idhaa zote za Radio Africa; Radio Jambo,  Classic 105, Smooth FM, Kiss 100, na Homeboyz Radio.

'Suzanna', ambacho ni kibao cha kwanza kwenye albamu hiyo inayotarajiwa kizinduliwa Februari  6 mwaka huu na kutamba katika ulingo wa mziki, kufikia sasa umevutia zaidi ya mashabiki milioni tisa  kwenye YouTube.

Kibao cha pili, 'Brighter Days', kilichozinduliwa Aprili 17, tayari kina ushabiki wa zaidi ya milioni 1.2 kwenye YouTube.

Sauti Sol wamesema kwamba kuzinduliwa kwa wimbo 'Insecure' kunaambatana na kujitolea kwao kuleta mwangaza na uchangamfu kupitia muziki wakati huu mgumu ("to brighten up these times of gloom and doom with music").

Walisema kwamba hali ya sasa ambapo kuna marufuku ya kutozuru nchi za kanda hii, kafyu nchini, watu kutotangamana na maruku ya safari za kimataifa, hali hii imesambaratisha biashara yao ya kutumbuiza watu.

"Imetulazimu sio tu kuahirisha au kufutilia mbali hafla za kimataifa na za humu nchini, bali pia kujitenga wakati huu ambao tunahitaji kuwa pamoja kujiandaa kwa uzinduzi wa albamu yetu mpya na kuinadi katika maeneo mbali mbali duniani," bendi hiyo ilisema.

Waliongeza kuwa ; "Ni matarajio ya mashabiki na wadau wetu kwamba tutazindua albamu hii kwa hafla ya kipekee licha ya hali ilivyo kwa sasa."

Kufuatia mashauriano na wizara ya Afya, bendi hiyo imejitenga pamoja na jamaa wengine watano wanaoshughulikia video yao.

Hatua hii itawezesha bendi hiyo, kujiandaa, kutengeza video ya kuzindua albamu hiyo na kujiandaa kwa hafla ya uzinduzi wa albamu hiyo.

Kampuni ya Radio Africa Group itashirikiana na Sauti Sol kwa safari hii kuhakikisha kwamba mashabiki wao ulimwenguni kote wanapokea muziki huu wakiwa nyumbani mwao.