Mashine ya kupima corona Tanzania 'yapatikana na hitilafu'

_107359610_umimwalimu
_107359610_umimwalimu
Wizara ya afya nchini Tanzania imetangaza kwamba uchunguzi wa serikali uliokuwa ukifanywa katika maabara kuu ya nchi hiyo umebaini kuwa moja ya mashime ya kupima corona ilikuwa na hitilafu.

Waziri Ummy Mwalimu hii leo ametangaza matokeo ya uchunguzi aliyoagiza kufanyika baada ya Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kutilia shaka ufanisi wa maabara hiyo.

"Kamati imebaini kuwepo kwa mapungufu ya uendeshaji wa kitaaluma katika upimaji wa vipimo na uhakiki wa ubora wa majibu'' amesema Waziri Mwalimu.

Pia kumebainika kuwepo kwa udhaifu katika uhifadhi wa vipimo vya covid-19, aidha imebainika kuwepo kwa upungufu wa Wataalamu"- Waziri Afya Ummy mwalimu amesema.

Wizara ya afya nchini humo imeweka wazi kwamba sasa vipimo vitakuwa vinafanyika katika maabara iliyopo mabibo.

"Kuanzia sasa shughuli zote za upimaji wa maabara ya taifa zitafanyika katika maabara mpya ya mabibo yenye vifaa vya kisasa vyenye ubora na uwezo wa kupima sampuli 1,800 ndani ya saa 24"- amesema Ummy Mwalimu.

Kulingana na wizara hiyo, maabara iliyotumika awali na kukutwa na mapungufu ilikuwa na uwezo wa kupima sampuli 300 kwa saa 24 na ilianzishwa mwaka 1968 katika ofisi za NIMR, mtaa wa Obama DSM, na sasa imeamamrishwa kupima magonjwa mengine.

Vipimo vinavyotumika kupima corona Tanzania havina hitilafu (CDC)

Pamoja na majibu hayo ya uchunguzi wa kamati maalum, Mei 7 Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (CDC) kilisema kwamba vifaa vya kupimia virusi vya corona nchini Tanzania havina shida yeyote.

"Vipimo ambavyo Tanzania inatumia tunajua kwamba vinafanyakazi vizuri," Dkt. John Nkengasong alisema hivyo katika mkutano na wanahabari wa njia ya mtandao.

Kauli hiyo ya Mkuu wa Africa CDC, inapingana na kauli ya rais wa Tanzania ambaye alisema huenda vipimo hivyo vikawa na matatizo.

Kituo hicho cha Africa CDC pamoja na wakfu wa Jack Ma, Shirika la msaada la bilionea wa China, lilisambaza vifaa hivyo, Nkengasong alisema na kuongeza kwamba viliidhinishwa na wanachojua ni kwamba vinafanyakazi vizuri.

-BBC