Pasta ageukia utapeli ili kupata lishe wakati huu wa janga la corona

Mchungaji kutoka eneo la Githunguini alijikaanga mwenyewe baada ya kuanza kuwahadaa waumini wake kuwa alikuwa na mafuta matakatifu ya kuwakinga na corona.

Nduru za taarifa zinaarifu kwamba baada ya serikali kutangaza kufungwa kwa makanisa ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona pasta alilazimika kubini mbinu nyingine ya kupata hela za kujikumu kimaisha.

Hata hivyo mbinu yake haikufaulu baada ya waumini wake kumtoroka baada ya kugundua kuwa alikuwa anawatapeli tu.

Taarifa hizo ziliarifu kuwa mchungaji huyo alikuwa anaenda akizungunga nyumbani mwa waumini hao na kuwapa mafuta ambayo alikuwa anawaambia ni kinga dhidi ya virusi vya corona.

Inasemkana ujanja wake wa siku chache ulifika kikomo alipokutana na afisa wa afya wa kijijini aliyetaka kujua tiba yake ilikuwa ni ya asili ipi.

Afisa huyo alimuarifu bosi wake ambaye kwa pamoja walaimuonya mchungaji dhidi ya kusaka hela kwa kuwapotosha watu akisingizia ana tiba ya corona.

Penyenye zinaarifu kuwa maafisa hao walitishia kumshtaki na kumchukulia hatua kali za kisheria kwa kukaidi maagizo ya kusambaa kwa maradhi ya Covid-19.

Duru zinaarifu waumini wake walianza kumhepa mmoja baada ya mwingine walipoigundua ajenda yake kuu ilikuwa ni kuwafyonza tu na wala sio kuwalisha neno la kweli.

Wahudumu wa afya walizidi kuwahimiza watu eneo hilo kuzingatia usafi kwa kunawa mikono, kuvaa maski, kuepuka misongamano ya watu ili kujiepusha na corona na wala sio kutapeliwa na manabii wa uongo.