Raila Odinga ajiunga na ulimwengu kupinga mauaji ya George Floyd Marekani

Kiongozi wa ODM, Raila Odinga ametumia kinukuu cha mwanaharakati wa Marekani Martin Luther King Junior kutaka haki ya wazi itendeke kutokana na mauaji ya George Floyd.

Raila alijiunga na ulimwengu mzima pamoja na familia kushinikiza haki kwa jamaa huyo mwenye miaka 46 baada ya kuuwawa na polisi huku akililia uhai wake.

Mjumbe huyo wa Muungano wa Afrika alitamani kuona taifa la Marekani likiwa bila ubaguzi wa rangi badala yake kuishi kulingana na ndoto ya Luther. 

"Ninajiunga na maelfu kuombea familia ya George Floyd na Marekani, maombi kuwa kutakuwepo haki na uhuru kwa binadamu wote ambao wanatambua Marekani kama taifa lao na wananchi hawabaguliwi kulingana na rangi yao ya ngizi

Ni ndoto ambayo Marekani itatimizia George na wananchi wote. Ni ndoto ambayo sisi Wafrika pia tuna deni kwa wananchi wetu huku tukisimama na familia ya Floyd nchini Marekani," Raila Aliandika.

Kigogo huyo wa siasa na Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo walikuwa viongozi wa kwanza kutoka Afrika kushtumu kifo cha Floyd ambacho kilifichua mauaji ya kiholela Marekani.

"Haiwezi kuwa sawa katika karne hii ya 21, Marekani yenye demokarisia, kuendelea kukumbana na ubaguzi wa rangi. Kwa niaba ya Ghana, ninatoa rambirambi zangu kwa familia na wapendwa wa marehemu George Floyd,"  Nana aliomboleza.

Afisa wa polisi aliyetambuliwa kama Derek Chauvin alinaswa kwenye video akiwa amemuwekea Floyd goti lake kwa dakika 10 nje kituo cha polisi Jumatatu, Mei 25.

Marehemu ambaye ni M'Marekani Mweusi aliaga dunia baadaye katika kizuizi cha polisi huku maafisa wa usalama wa Minneapolis wakidai alifariki kutokana na matitizo ya kimatibabu.

Ni kitendo ambacho kiliwagadhabisha wananchi na viongozi wengi kwa jumla huku wakitaka haki kutendeka.