Mgogoro: Mabilioni ya Chama cha Jubilee yazua mgawanyiko zaidi katika ‘talaka’ ya Uhuruto

Makabiliano kati ya kambi za  rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto sasa yameelekea katika mfuko wa fedha za chama hicho huku upande wa Ruto ukiushtumu mrengo wa rais Kenyatta  kwa utumizi  mbaya wa fedha na hata ufisadi.

Katika kinachonekana kama kudorora zaidi kwa uhusiano kati ya viongozi hao wawili , washirika wa Ruto wanaoshikilia nafasi za uongozi chamani, wanasema chama hicho kilitoa zaidi ya shilingi milioni 183  mwaka wa 2018 ambazo matumizi yake hayajaelezwa ifaavyo.

Naibu katibu mkuu wa chama Caleb  Kisitany ambaye ni mshirika wa Ruto ametaka kupewa stakabadhi za keleza jinsi mamilioni hayo yalivyotumiwa  lakini katibu mkuu Raphael Tuju amempepezea chini akisema  matakwa yake hayo ni sarakasi tu za kisiasa kwa sababu hana uwezo au mamlaka ya kutaka kuchunguza  madai hayo.

Kositany anataka kupewa stakabadhi mbalimbali zikiwemo taarifa za benki za  akaunti za pesa za Chama cha Jubilee kwa muda wa miaka  4 iliyopita. Yadaiwa Kositany ni miongoni mwa washirika wa Ruto watakaopigwa shoka kutoka nafasi za uongozi katika chama cha Jubilee.

Kositany ameshangaa mbona chama hicho kinalipa kodi ya jengo zima la makao makuu ya Jubilee ilhali hakitumii jengo zima na pia kuhoji kutolewa kwa mamilioni  ya pesa kulipa kodi za matawi ya chama ilhali hayajakuwa yakiendelea na oparesheni  zozote.

Wawakilishi wa kaunti wa  Chama cha Jubile  wamekuwa wakitoa shilingi 5000 kila mwezi, wabunge elfu 20  na magavana shilingi elfu 50 kila mwezi kwa chama hicho kwa miaka saba iliyopita.

Chama hicho kina  wabunge 171  katika mabunge yote mawili hatua inayomaanisha kwamba wamekuwa wakikusanya  shilingi milioni 3.4 kila mwezi. Magavana wote  25  wa Jubilee  hutoa pato la shilingi millioni1.2 kila mwezi  kando na mamia ya wawakilishi wa kaunti  ambao pia hutoa michango yao chamani.

Wabunge wake watano wa EALA hutoa shilingi 20,000 kila mwezi.  Hatua ya kutaka stakabadhi za kifedha za chama imejiri baada ya washirika wa Ruto chamani humo kupa kusalia ndani ili kuendeleza mapambano yao wakiwa ndani ya Jubilee.