Wakati wa kufunguliwa kwa shule umetimia - Magoha

Taarifa ya Luke Awich

Waziri wa elimu George Magoha amewaambia wabunge kwamba wakati umetimia kufunguliwa kwa shule.

Waziri aliambia kamati ya bunge kuhusu elimu kwamba watawapa kipau mbele wanafunzi wa kidato cha nne na darasa la nane katika awamu ya pili ya kufunguliwa kwa taasisi za elimu itakayotangazwa hivi karibuni.

Waziri bila kutaja tarehe za kufunguliwa kwa shule, alisema muda umewadia kwa taifa kufungua shule akitaja mifano ya nchi jirani ambazo zimeruhusu wanafunzi kurejea shuleni baada ya janga la Covid-19.

Alitaja nchi kama vile Zambia na Angola ambazo zimeruhusu wanafunzi kurejea shuleni baada ya kudhibiti janga la corona.

Alisema kwamba huenda hali ya covid-19 haitabadilika siku za usoni.

“Ni wakati wa kufungua na kama vile rais alisema, tunahitaji tu kujua ni vipi.  Siwezi kuwapa tarehe lakini nataka kuwahakikishia kwamba taifa la Kenya linachukuwa kila tahadhari. Kile tunafaa kujiuliza ni kwamba nini kitakuwa tofauti mwezi Januari 2021?” Magoha aliuliza.

Magoha alikiri kwamba itakuwa vigumu kutimiza matakwa ya umbali wa mita moja lakini alielezea imani yake kwamba kuzingatia kanuni zingine kama vile kuvalia maski na kuosha mikono kutasaidia wanafunzi kuwa salama shuleni.

Anasema wataangalia wanafunzi katika vyuo vikuu na taasisi zingine za kadri kabla ya kuamua hatua itakayo fuata.

Akihutubia taifa katika hotuba yake ya 12 kuhusu janga la Covid-19, rais Uhuru Kenyatta alimtwika jukumu waziri wa elimu kutoa muongozo wa kufunguliwa kwa taasisi za elimu zikiwemo shule na kuhakikisha kwamba mazingira shuleni ni salama kwa watoto.

Soma habari zaidi hapa;