Wazazi waanza kujiandaa kwa shule kufunguliwa

Baada ya waziri wa elimu George Magoha kutangaza kwamba shule zitafunguliwa hivi karibuni, wazazi sasa wameanza mikakati ya kujiandaa kurejesha watoto wao shuleni.

Wazazi wengi hata hivyo wameelezea hofu yao kuhusu watakako pata pesa za kuwalipia wanao karo shule zitakapofunguliwa.

"Mimi nilipoteza kibarua changu, baada ya boss wangu kufunga kazi kutokana na athari za corona, sasa hivi sijui hata watoto wangu watakula nini na sasa wakifungua shule pesa ya kuwapa nauli itatoka wapi," alisema mzazi mmoja.

Wazazi wengi wamelalamikia kutokuwa na pesa za kuwarejesha wanao shuleni baada ya watu wengi kupoteza ajira huku baadhi yao wakipunguziwa mishahara kutokana na athari za virusi vya corona.

Waziri wa elimu George Magoha mapema wiki hii aliwambia wabunge kwamba wakati umetimia kufunguliwa kwa shule.

Waziri aliambia kamati ya bunge kuhusu elimu kwamba watawapa kipau mbele wanafunzi wa kidato cha nne na darasa la nane katika awamu ya pili ya kufunguliwa kwa taasisi za elimu itakayotangazwa hivi karibuni.

Waziri bila kutaja tarehe za kufunguliwa kwa shule, alisema muda umewadia kwa taifa kufungua shule akitaja mifano ya nchi jirani ambazo zimeruhusu wanafunzi kurejea shuleni baada ya janga la Covid-19.

“Ni wakati wa kufungua na kama vile rais alisema, tunahitaji tu kujua ni vipi. Siwezi kuwapa tarehe lakini nataka kuwahakikishia kwamba taifa la Kenya linachukuwa kila tahadhari. Kile tunafaa kujiuliza ni kwamba nini kitakuwa tofauti mwezi Januari 2021?” Magoha aliuliza.

Magoha alikiri kwamba itakuwa vigumu kutimiza matakwa ya umbali wa mita moja lakini alielezea imani yake kwamba kuzingatia kanuni zingine kama vile kuvalia maski na kuosha mikono kutasaidia wanafunzi kuwa salama shuleni.

Akihutubia taifa katika hotuba yake ya 12 kuhusu janga la Covid-19, rais Uhuru Kenyatta alimtwika jukumu waziri wa elimu kutoa muongozo wa kufunguliwa kwa taasisi za elimu zikiwemo shule na kuhakikisha kwamba mazingira shuleni ni salama kwa watoto.

Soma habari zaidi hapa;