Sitajisalimisha, Ndindi Nyoro asema

Muhtasari

• Nyoro siku ya Jumanne alishtumu ofisi ya rais akisema kwamba inatumika kuwatishia viongozi fulani.

•  Idara ya DCI inaamini kwamba wawili hao na viongozi wengine walihusika kupanga vijana waliozua rabsha katika eneo la Kenol siku ya Jumapili.

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro
Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro
Image: HISANI

 Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ameshikilia  kwamba hatajisalimisha kwa polisi.

Nyoro siku ya Jumanne alishtumu ofisi ya rais akisema kwamba inatumika kuwatishia viongozi fulani.

Nyoro na mwenzake wa Kandara Alice Wahome siku ya Jumatatu waliagizwa kufika afisi za DCI kuhusiana na rabsha zilizoshuhudiwa katika eneo la Kenol ambapo watu wawili walifariki na wengine wengi kujeruhiwa.  

Idara ya DCI inaamini kwamba wawili hao na viongozi wengine walihusika kupanga vijana waliozua rabsha katika eneo la Kenol siku ya Jumapili.

Inspekta mkuu wa polisi Hillary Mutyambai akitoa agizo la kukamatwa kwao alisema kwamba magari yaliyotumika kusafirisha vijana hao yatasakwa na kuzuiliwa ili kusaidia katika uchunguzi.

Tukio hilo lilifanyika siku ya Jumapili kabla ya kuwasili kwa naibu rais William Ruto na wandani wake. 

Lakini baadaye Nyoro na Wahome walipuuzilia mbali agizo la kuandikisha taarifa wakisema polisi walikuwa hawajawapa agizo rasmi la kujiwasilisha.

Akihojiwa kwenye Citizen TV, Nyoro alishtumu serikali kwa kufadhili vijana kuvuruga mkutano wa kuchangia kanisa pesa. 

"Wacha niwaeleze kwa kinaga ubaga. Sitajiwasilisha kwa polisi yeyote. Sitatumika na wauaji kusafisha makosa yao..... wako na 'system' wanaweza kufuatilia simu yangu wanajua safari zangu za kila siku,"  alisema.

Mwakilishi wa wanawake wa Homa Bay Gladys Wanga hata hivyo, amemtaka Nyoro kujiwasilisha kwa polisi na kuandikisha taarifa kuhusu kile anajua kuhusu vurugu.

Wanga alisema kwamba inasikitisha kuwa mbunge huyo analeta sarakasi katika kisa hicho ili watu wamuonee huruma.