Penzi sumu:Jamaa aliyekiri kumuua mpenzi wake ataka korti kuharakisha hukumu yake

Muhtasari
  • Jamaa aliyekiri kumuua mpenzi wake ataka korti kuharakisha hukumu yake
  • Karani alidaiwa kumuua Nyokabi Aprili 14 baada ya wawili hao kukorofishana
Pingu
Image: Radio Jambo

Mshukiwa mkuu katika mauaji ya Catherine Nyokabi, atasalia kizuizini kwa siku 14 zingine ili polisi wazidi kuchunguza mauaji hayo.

Evans Karani alipelekwa katika  korti ya Thika mbele ya hakimu Oscar Wanyaga,ambaye aliwaruhusu polisi kumtia korokoroni.

Karani alidaiwa kumuua Nyokabi Aprili 14 baada ya wawili hao kukorofishana.

" Ningependa utoe kifungo changu ili nianze hukumu yangu mapema," Karani aliambia mahakama.

Akiyajibu madai hayo, hakimu huyo alikuwa na haya ya kusema," Nitapeana hukumu yangu wakati ufaao, natumai unanielewa vema."

Mshukiwa aliyasema haya baada ya mahakama kupeana siku 14 zaidi ili uchunguzi zaidi ufanywe kuhusiana na kesi hiyo.

Baba ya marehemu, Gitonga Njogu, aliliambia gazeti moja kuwa ripoti za awali zilidokeza binti yake, mzaliwa wa kwanza katika familia ya watoto wanne, alikufa katika ajali ya barabarani.

"Kwenye mitandao ya kijamii, watu fulani walikuwa wakidai mtoto wangu aliuawa katika ajali ya gari huko Juja

Hata hivyo, tulipoona mwili wake kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Jiji, tulishtuka. Majeraha yanayoonekana yalionyesha wazi sababu ya kifo cha Nyokabi haikuwa ajali ya barabarani kama ilivyodaiwa, "Njogu alisema.

Alisema Nyokabi alikuwa akifanya kazi kwa bidii, mchangamfu na mwenye upendo sana na mustakabali mzuri.