Muthama Kuwania Kiti cha Ugavana Machakos kwa Tiketi ya Chama cha UDA

Muhtasari
  • Muthama atangaza kuwania kiti cha ugavana Machakos 2022

Aliyekuwa seneta wa Machakos Johnstone Muthama ametangaza kwamba atakuwa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania kiti cha cha ugavana wa Machakos 2022.

Kupitia kwenye ukurasa wake wa Twitter, Muthama alisema wakazi wa Machakos wamekuwa wakimrai arejee uongozini.

" Tangu mwaka wa 2017 nilipochukua likizo katika siasa, nimekuwa nikipokea jumbe kutoka kwa wakazi wa Machakos wakinirai kwamba nirejee uongozini, iwapo hilo ndio ombi lao basi sina budi ila kuwahudumia wanavyotaka," Alisema Muthama.

Muthama alitangaza kwamba alikuwa  amechukua mapumzika kutoka kwa siasa baada ya kuwa seneta wa kwanza wa Machakos kati ya 2013 na 2017.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka aligombana na Muthama ambaye alikuwa mshirika wake muhimu na mfadhili wa chama baada ya kukataa kufanya kazi na Naibu Rais William Ruto, muungano ambao Muthama alikuwa akiuunga mkono sana.

Mnamo Januari mwaka jana, Muthama alitangaza kwamba makubaliano ya Ruto-Kalonzo yalikuwa karibu lakini Makamu wa Rais wa zamani alitupilia mbali madai hayo.

Muthama alikuwa akifanya mazungumzo ya kimya kimya na Ruto ili kumleta Kalonzo lakini alikataa mikataba na badala yake akasaini makubaliano ya ushirikiano na chama cha Rais Uhuru Kenyatta cha Jubilee.