Acheni kutumia bunduki zenu vibaya! Uhuru awaambia polisi

Muhtasari
  • Rais Uhuru Kenyatta amewasihi polisi wasitumie vibaya bunduki zao
  • Uhuru alisema ni bora kushughulikia masuala kuliko kuua watu
Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amewasihi polisi wasitumie vibaya bunduki zao.

Akizungumza wakati wa gwaride la GSU Jumatano, Uhuru aliwataka polisi kuzungumzia matatizo yao ya kifamilia na sio kuchukua bunduki.

"Mambo ni mengi lakini hakuna shida haiwezi kutatuliwa watu wakiongea..," Alisema Uhuru.

Uhuru alisema ni bora kushughulikia masuala kuliko kuua watu.

"Kama kitu kinakusumbua unaweza kuongelesha wenzako. Mashida ni mingi . Afya ya akili ni tatizo lakini inaweza kushughulikiwa unapofikia," alisema.

"Bunduki yako ni ya ulinzi isichukue maisha...tatizo hili lipo na tunataka kulishughulikia. Lakini ninakusihi, ikiwa una tatizo nyumbani au kazini, tafuta mtu wa kuzungumza naye."

Uhuru alisema wanaweza kuzungumza na wanafamilia au hata wakuu wa polisi walio karibu.

“Mtapata suluhu kwa kuzungumza nao hakuna jambo ambalo haliwezi kutatulika hakuna haja ya kufanya mnachofanya, tatizo hili tunalo na ni sehemu yetu tafadhali piga hatua mbele,” alisema.

"Hakuna aibu ndani yake.. tunaweza kukusaidia kutatua tatizo lako na kuwa hata afisa bora."

Alikuwa akimjibu konstebo Benson Imbatu aliye katika kituo cha polisi cha Kabete ambaye alienda nyumbani na bunduki yake aina ya AK47 na kugombana na mkewe Carol Imbatu.

Afisa wa polisi aliwapiga risasi na kuwaua watu sita kabla ya kujitoa uhai katika eneo la Kabete Nairobi katika kisa cha kushangaza.

Waliofariki ni pamoja na mkewe, majirani na waendesha bodaboda ambao walikuwa wamekimbilia nyumbani kwake kuangalia kilichojiri waliposikia milio ya risasi Jumanne asubuhi.