Fahamu jinsi ya kupata Hustler Fund na kukuza viwango vya mkopo

Wakopaji wa Hustler Fund watatumia *254# kupata Hustler fund.

Muhtasari

•Wakenya ambao wamejisajili kwa Safaricom, Airtel na Telekom watahitajika kubonyeza *254#  ili kupata mikopo.

•Waziri Chelugui alisema kuwa wafanyikazi watahitaji tu simu zao, kwani hakutakuwa na mawakala wa mchakato huo.

Image: HISANI

Wakopaji wa Hustler Fund watatumia *254# kupata mkopo huo, kampuni za mawasiliano zinazoongoza zimetangaza.

Wakenya ambao wamejisajili kwa Safaricom, Airtel na Telekom watahitajika kubonyeza kodi hiyo fupi ili kupata mikopo baada ya kuzinduliwa na Rais William Ruto.

Kuanzia siku ya Jumatano, Wakenya wataweza kupata mikopo ya Hustler Funds kupitia simu zao za rununu.

Kwa sasa, kiwango cha chini ambacho mkopaji anaweza kupata ni Ksh 500 ilihali cha juu zaidi ni na Sh50,000.

Hata hivyo, mnamo wakati wa uzinduzi, Rais William Ruto alisema wakopaji wana nafasi ya kuongeza kiwangi cha mikopo yao iwapo watarejesha mikopo yao kabla ya siku ya mwisho ya kurejesha iliyotolewa kufika.

“Wakati unakopa na kulipa ndio unapata nafasi nyigine ya kukopa tena, unahitimu uende micro loan, utoke Sh50,000 uende level nyigine,” alisema.

Akizungumza na wanahabari, Waziri wa Vyama vya Ushirika na Maendeleo ya SMEs Simon Chelugui alisema viwango vya mikopo vitaongezeka kulingana na tabia ya mkopaji.

"Kiwango kitapitiwa upya na kurekebishwa kulingana na historia ya ukopaji na urejeshaji wa mikopo ya awali iliyochukuliwa," alisema.

Historia ya mkopo ya mkopaji pia itaamua kiasi ambacho mtu atapokea.

"Hustlers wanahimizwa kuendelea kutumia Mfuko na kulipa mikopo yao kwa wakati, ili kuongeza ukomo wao."

 Chelugui alisema hakutakuwa na usajili unaohitajika kwa Huster Fund. Alisema wakopaji watatumia kodi fupi ya SMS ambayo itawaelekeza kwenye menyu fulani, ambayo itawongoza hadi kwenye usajili wa mkopo.

“Tunawaomba wananchi kupuuza aina zote za mawasiliano ambapo wanaaalika kujiandikisha kupata fedha kwenye tovuti au kupitia namba ya simu,” alisema.

Aliongeza kuwa wafanyikazi watahitaji tu simu zao, kwani hakutakuwa na mawakala wa mchakato huo.

 “Fedha hizo zitapatikana kupitia namba za simu na mitandao husika,” alisema. 

Waziri pia alitangaza kuanzishwa kwa kituo cha simu ambacho kitajibu maswala na maswali ya wakopaji.

Aliongeza kuwa kituo hicho kitakuwa hai pindi mradi huo utakapozinduliwa.  

Kupitia Hustler Fund, kila mara mtu anapokopa kiasi, Chelugui anasema 5% ya pesa hizo zitaenda kwenye mpango wa kuweka akiba, ambapo pesa hizo huongeza riba.

"Kwa kila Sh2 itakayowekwa, serikali itaongeza shilingi moja."