Ugonjwa wa saratani wa gwiji Brazil Pele umesambaa, hospitali yasema

Pele amekuwa hospitalini kwa zaidi ya wiki tatu.

Muhtasari

•Binti yake alisema kwenye mtandao wa kijamii kwamba atasalia hospitalini wakati wa Krismasi.

•Pele aliondolewa uvimbe kwenye utumbo wake mnamo Septemba 2021 

Gwiji wa soka wa Brazil Pele
Image: BBC

Saratani ya nguli wa Brazil Pele imesambaa, kulingana na hospitali ambayo nyota huyo wa zamani wa soka mwenye umri wa miaka 82 anatibiwa.

Mshindi huyo mara tatu wa Kombe la Dunia amekuwa hospitalini kwa zaidi ya wiki tatu.

Binti yake alisema kwenye mtandao wa kijamii kwamba atasalia hospitalini wakati wa Krismasi.

Hospitali ya Israelta Albert Einstein ilisema Pele "anaonyesha kusambaa kwa ugonjwa wa saratani na anahitaji uangalizi mkubwa kuhusiana na matatizo ya figo na moyo".

Pele aliondolewa uvimbe kwenye utumbo wake mnamo Septemba 2021 na tangu wakati huo amekuwa akitibiwa mara kwa mara.

"Krismasi yetu nyumbani imesimamishwa," aliandika bintiye Pele, Kely Nascimento, kwenye Instagram.

Mara tu baada ya kulazwa, hospitali ya Sao Paulo ilisema Pele "alikuwa na mwitikio mzuri wa matibabu ya maambukizo ya upumuaji" na kuongeza kuwa alikuwa akifanyiwa "tathmini upya ya matibabu ya chemotherapy".