Aliyekuwa Waziri wa Elimu, George Magoha ampoteza kaka

Mwezi Agosti 2021, Magoha alimpoteza kaka yake mwingine, Charles Agunga Magoha aliyefariki nchini Uswidi.

Muhtasari

•Kulingana na tangazo kwenye gazeti moja la hapa nchini, Nyabera alifariki katika jiji la Allen, jimbo la Texas nchini Marekani mnamo Desemba 6, 2022.

•Magoha alipata kazi mpya katika Chuo Kikuu cha Maseno kama profesa wa Upasuaji katika kitengo cha Tiba.

Marehemu Alex Nyabera Magoha
Image: HISANI

Aliyekuwa waziri wa elimu George Magoha yuko katika hali ya majonzi kufuatia kifo cha kaka yake Alex Nyabera Magoha.

Kulingana na tangazo kwenye gazeti moja la hapa nchini, Nyabera alifariki katika jiji la Allen, jimbo la Texas nchini Marekani mnamo Desemba 6, 2022.

Hata hivyo, sababu ya kifo chake haijawekwa wazi.

"Mwili wa marehemu utaondoka katika Chumba cha Kuhifadhi Maiti cha  Hospitali ya Aga Khan Kisumu mnamo Jumamosi, Januari 28, 2023 kwa misa ya ukumbusho katika Shule ya Msingi ya Yala Township Yala ikifuatiwa na maziko nyumbani kwake Umiru, Yala, kaunti ndogo ya Gem," sehemu ya tangazo hilo ilisomek.

Mwezi Agosti 2021, Waziri huyo alimpoteza kaka yake mwingine, Charles Agunga Magoha aliyefariki nchini Uswidi.

Magoha alihudumu kama Waziri katika serikali ya Uhuru kabla ya Waziri wa sasa Ezekiel Machogu kuchukua wadhifa kufuatia mabadiliko yaliyofanywa na Rais William Ruto baada ya kuchukua hatamu.

Mapema wiki hii, Magoha alipata kazi mpya katika Chuo Kikuu cha Maseno kama profesa wa Upasuaji katika kitengo cha Tiba.

Katika mahojiano na wanahabari mnamo Agosti 2022, Magoha alikuwa amedokeza kurudi katika kliniki yake katika Hospitali ya Nairobi.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Elimu mnamo Machi 2019, alihudumu kama mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Elimu Kenya (KNEC)

Pia aliwahi kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Nairobi kati ya 2005 na 2015.