Kijana wa miaka 17 apatikana na hatia ya kumnajisi msichana wa miaka 5 Kajiado

Mahakama iligundua kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kesi hiyo.

Muhtasari

•Mshtakiwa alipatikana na hatia ya shtaka kwamba mnamo Januari 23, 2023 alimnajisi msichana wa miaka mitano.

•Mhasiriwa alisema baada ya mamake kuondoka, alienda kwa nyumba ya mshtakiwa na akamlaza kwenye kochi na kumnajisi.

Mahakama
Mahakama

Mahakama ya Loitoktok imempata mvulana wa miaka 17 na hatia ya kumnajisi msichana wa miaka mitano.

Mshtakiwa ambaye alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Judicastor Nthuku alipatikana na hatia ya shtaka kwamba mnamo Januari 23, 2023 katika kijiji cha Ilasit katika Kaunti Ndogo ya Loitoktok, alimnajisi msichana huyo wa miaka mitano.

Kulingana na Mercy Njeri, mamake msichana huyo, siku hiyo alimwacha bintiye nyumbani akienda kazini baada ya kukosa kwenda shule kwa kuumwa na jino.

Aliporudi na alipokuwa anamuogesha bintiye jioni, mtoto huyo alianza kupiga kelele na baada ya kumuuliza, msichana huyo alimwambia mchana, alikuwa ameenda nyumbani kwa mshtakiwa ambako alimnajisi.

Mara moja, Njeri na jirani yake walikwenda kwa Ngomi lakini wakamkosa.

Msichana huyo aliiambia mahakama jinsi siku ya tukio, baada ya mamake kuondoka, alienda kwa nyumba ya mshtakiwa na akamlaza kwenye kochi na kumnajisi.

Siku iliyofuata, kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Ilasit huku mtoto huyo akipelekwa katika kituo cha afya kilicho karibu kwa uchunguzi wa kimatibabu.

Baadaye, polisi wakishirikiana na Njeri na msichana huyo walienda kwa nyumba ya mshtakiwa, wakamkamata, wakamsindikizwa hadi kituo cha polisi na kumshtaki kwa kosa hilo kisha kufikishwa mahakamani ambapo alikanusha shtaka hilo.

Katika utetezi wake, mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo akisema kuwa siku hiyo alikaa kwa rafiki yake na kukamatwa siku iliyofuata.

Hata hivyo, mahakama iligundua kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kesi hiyo bila shaka na kesi hiyo ilipangwa kutajwa Mei 29 kusubiri ripoti ya awali ya hukumu.