Waziri Kipchumba Murkomen azua wasiwasi kwa kauli 'Rwanda ina utawala wa kiimla'

Murkomen alipuuzilia mbali kulinganishwa kwa Kenya na Rwanda akisema hali ya kisiasa Rwanda ni tofauti na demokrasia nchini Kenya.

Muhtasari

•Murkomen amezua utata baada ya kusema kuwa Rwanda ina "utawala wa kiimla" ambapo "kila anachosema rais ni sheria".

•Baadhi ya Wakenya wameita kauli ya Murkomen "mazungumzo ya baa" ambayo yanaweza kuzua mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili za Afrika Mashariki.

Waziri Kipchumba Murkomen
Image: MAKTABA

Waziri wa barabara na uchukuzi Kipchumba Murkomen amezua utata baada ya kusema kuwa Rwanda ina "utawala wa kiimla" ambapo "kila anachosema rais ni sheria".

Murkomen alikuwa akijibu ukosoaji ambao ulilinganisha isivyofaa mfumo wa usafiri wa Kenya na ule wa nchi ambayo ni jirani wa karibu [Rwanda]

Rwanda, ambayo hapo imekuwa na uhusiano mzuri na Kenya, bado haijajibu maoni ya waziri.

Wakenya walimsihi Bw Murkomen kubatilisha matamshi hayo wakihofia kuwa wataichokoza Rwanda bila sababu.

Akionekana moja kwa moja kwenye televisheni ya kibinafsi ya Citizen Jumatatu usiku, Bw Murkomen aliulizwa ni kwa nini Kenya haijaweza kuifanya sekta ya uchukuzi wa umma kufanya kazi kwa utaratibu kama wa Rwanda.

Nchini Kenya, mabasi madobo ya kibinafsi ya abiria yanayokiuka kanuni ambazo hupita katika barabara zenye msongamano mara nyingi huwa chanzo cha ajali.

Lakini waziri wa uchukuzi alipuuzilia mbali kulinganishwa kwa Kenya na Rwanda akisema kuwa hali ya kisiasa nchini Rwanda ni tofauti na demokrasia nchini Kenya.

"Rwanda si kama Kenya. Rwanda ni serikali ya kiimla na huko chochote anachosema rais ni sheria," alisema waziri Murkomen, akiongeza kuwa Rwanda "ni ndogo hata kuliko kaunti ya Kajiado", kaunti iliyoko viungani mwa Nairobi.

"Kwa kila uamuzi unaoufanya katika nchi hii lazima upitie pendekezo kisha bunge kisha umma ushirikishwe," aliongeza.

Rais wa Rwanda Paul Kagame amekuwa mkuu wan chi hiyo tangu mwaka 1994. Alishinda uchaguzi uliopita wa urais kwa karibu asilimia 99 ya kura na, uchaguzi ukiruhusu, anaweza kusalia madarakani hadi 2034. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameishutumu serikali yake kunyamanzisha sauti za upinzani ,shutuma ambazo zinakunushwa.

Kauli za waziri huyo zilizua hisia kali kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya Wakenya wakiziita "mazungumzo ya baa" ambayo yanaweza kuzua mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili za Afrika Mashariki.

Inavyoonekana akifahamu kwamba maoni yake tayari yalikuwa yakipata ukosoaji alipokuwa hewani, waziri huyo baadaye alimwambia aliyemhoji kuwa "utawala wa kiimla si jambo baya". Alisema mfumo wa uongozi wa Rwanda unampa mamlaka rais, ambaye alikuwa ameutumia "kwa manufaa chanya".

"Waziri Murkomen hawezi kushambulia nchi yenye urafiki huru bila uchochezi na kumdharau Rais Paul Kagame namna hiyo," wakili mashuhuri Ahmednasir Abdullahi alichapisha kwenye X baada ya kipindi kurushwa hewani.

Huku akionekana kudharau ukosoaji huo, Korir Sing'oei, afisa mkuu katika wizara ya mambo ya nje ya Kenya, alisema Rwanda ni "taifa muhimu ndugu" na "uongozi shupavu wa Rais Kagame unapendwa ndani na nje ya nchi".

Akijibu kuhusu X, Bw Sing'oei alisema kuna "kujieleza kwa njia mbali mbali " ndani ya nchi za Afrika Mashariki.

Baada ya kunyamaza, baadaye waziri wa uchukuzi alichapisha ujumbe kwenye X Jumanne asubuhi kwamba: "Mtindo wetu wa uongozi una mambo mengi mazuri lakini ni wa urasimu kupita kiasi."

Bw Murkomen, ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais William Ruto, hivi majuzi amekuwa akikosolewa kutokana na hitilafu ya umeme katika uwanja mkuu wa ndege wa Kenya jijini Nairobi.

Matamshi yake kuhusu Rwanda yamekuja siku moja tu baada ya Rais Ruto kusema uhusiano wa kidiplomasia wa Kenya na majirani zake ni "imara".

Rais Ruto alikuwa akijibu kuhusu wasiwasi kwamba huenda marais wa Afrika Mashariki walisusia sherehe za uhuru wa Kenya wiki iliyopita.