Video ya wanaume wakitishia kuwaua wanawake yazua hasira miongoni mwa Wakenya (+video)

Wanaume hao wameendelea kupokea shutuma nyingi kutoka kwa Wakenya huku wengi wakitaka kukamatwa kwao.

Muhtasari

•Boniface Mwangi alitumia fursa hiyo kuwaomba wanaume wengine wajiunge katika maandamano ya kupinga mauaji ya wanawake.

•"Mtakufa! Mtakufa! Nyie wanawake mtakufa niwaambieni. Ati pesa unataka ya mwanaume. Mtakufa sana.” Mwanaume mmoja alisema.

Image: TWITTER// BONIFACE MWANGI

Video ya wanaume wawili wakizungumza vibaya kuhusu wanawake na hata kutoa vitisho vya kutisha dhidi yao imekuwa ikivuma sana kwenye mitandao ya kijamii.

Wanaume wawili wasiojulikana kwenye video hiyo inayoonekana kurekodiwa katika bustani ya Jevanjee, jijini Nairobi wakati wa maandamano ya amani dhidi ya mauaji ya wanawake siku ya Ijumaa wameendelea kupokea shutuma nyingi kutoka kwa Wakenya huku wengi wakitaka kukamatwa kwao.

Mwanaharakati maarufu wa Kenya Boniface Mwangi alishiriki video hiyo kwenye akaunti yake ya Twitter na akatumia fursa hiyo kuwaomba wanaume wengine wajiunge katika maandamano ya kupinga mauaji ya wanawake.

“Hii ndiyo sababu sisi kama wanaume wa Kenya tunapaswa kuzungumza kwa ujasiri, na kwa sauti kubwa dhidi ya mauaji ya wanawake #EndFemicideKE. Wanaume hawa wawili kwa chuki wanawaambia wasichana hawa, “Tutawauua!” Boniface Mwangi alisema chini ya video aliyochapisha Ijumaa jioni.

Aliongeza, “Kama mwanamume na baba, wanaume hawa hawazungumzi kwa ajili ya wanaume ninaowajua. @WilliamsRuto sauti yako iko wapi? #ShutDownKE.”

Katika video hiyo, mmoja wa wanaume hao alisikika akipinga maandamano ya amani ya wanawake wanaotetea kukomeshwa kwa visa vilivyokithiri vya mauaji ya wanawake.

Mwanaume huyo alisikika akisema kuwa hata wanaume wameteseka sana mikononi mwa wanawake wanaodaiwa kuwapora pesa zao.

“Tutawaua! Tutawaua! Wengi iwezekanavyo,” Mmoja wa watu hao wawili alisikika akisema.

Mwanaume mwingine aliyekuwa amesimama karibu naye alisikika akimuunga mkono kwa kusisitiza kuwa watamaliza maisha ya wanawake.

“Hebu niwaambie, siwezi kukupeleka kwenye Pizza ukale pesa zangu.. C’mon, No way. Mtakufa! Mtakufa! Nyie wanawake mtakufa niwaambieni. Ati pesa unataka ya mwanaume. Mtakufa sana.” aliongeza.

Waliendelea kusema kuwa visa vya hivi majuzi vya mauaji ya wanawake ni sehemu ndogo tu, na kutishia kuwa wanawake wengi zaidi watapoteza maisha yao.

Video hiyo imepokea lawama nyingi kutoka kwa Wakenya na wamekuwa wito mwingi wa kukamatwa kwa wahusika.