Dp Gachagua amuomba radhi mama mwanzilishi wa taifa Mama Ngina Kenyatta

Muda mfupi uliopita baada ya kura za 2022, Dp Gachagua alimkabili Mama Ngina katika rabsha za kisiasa mara kadhaa huku akimlenga rais wa zamani Uhuru Kenyatta, mwanawe.

Muhtasari
  • Akizungumza kutoka nyumbani kwake Karen mnamo Jumatatu Machi 25, Gachagua alimsihi aliyekuwa mke wa rais wa Kenya kuwasamehe vyama vya siasa kwa kumpaka matope wakati wa kampeni.
Rigathe Gachagua na Mama Ngina
Image: Hisani

Naibu rais Rigathi Gachagua ameomba msamaha kwa aliyekuwa mke wa rais Mama Ngina Kenyatta kwa kile alichokitaja kuwa siasa mbaya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Akizungumza kutoka makao yake ya  Karen siku ya Jumatatu Machi 25, Gachagua alimsihi mama Ngina ambaye pia ni mama wa rais wa tano wa Kenya kuwasamehe wale wote waliyompaka matope wakati wa kampeni.

"Samahani kwa kumhusisha Mama Ngina Kenyatta katika siasa za uchaguzi mkuu uliopita. Yeye ni mama yetu na kwa hivyo ninaomba msamaha kwa niaba ya timu yetu kwa usumbufu wowote uliosababishwa kwake. Sitakubali kamwe mtu yeyote kumdhalilisha yeye au mtu yeyote kutoka eneo hili", Gachagua alisema wakati wa mahojiano yake na Kameme.

"Rais wa Zamani Uhuru Kenyatta ni mtoto wetu. Tulifanya kazi pamoja kwa miaka 17 na tulitofautiana kwa miaka 2 tu na sasa hiyo ni siku zilizopita. Ninamuombea katika kustaafu kwake. Uhuru ni mmoja wetu. Tutazungumza na kila mtu".

Gachagua pia alitoa wito kwa viongozi kukumbatia umoja ndani ya eneo la Mlima Kenya na nchini.

"Umoja wetu ndio nguvu yetu na ndio maana naendelea kusisitiza kwamba kizazi chetu kilindwe. Wakati wowote tukiwa serikalini tunatakiwa kuwa na umoja katika kufikiri na kupendana".

Muda mfupi uliopita baada ya kura za 2022, Dp Gachagua  alimkabili Mama Ngina katika rabsha za kisiasa mara kadhaa huku akimlenga rais wa zamani Uhuru Kenyatta, mwanawe.

Wakati wa hotuba ya hadhara katika Kaunti ya Nyeri, alimtaka Mama Ngina kusalimisha nusu ya shamba la Kenyatta kwa Mau Mau na watoto wao ambalo alidai lilinyakuliwa.

"Tunachoomba ni kuwasaidia Mau Mau kwa njia ya maana. Ardhi yote waliyochukua kutoka Mau Mau, warudishe angalau nusu ya sehemu za ardhi kwa Mau Mau na watoto wao pamoja na mimi. "