Charles Wambua: Mwanaume aliyeongoza utoajii wa miili katika eneo la taka la Kware azungumza

Hii si mara ya kwanza kwa Wambui kuhusika katika kutoa miili kutoka eneo hilo la kutupia taka.

Muhtasari

•Wambua alisema hapo awali alihusika katika utoaji wa miili iliyotupwa katika machimbo hayo mwaka mmoja uliopita.

•Wambua alizitaka mamlaka husika kutoa zana muhimu za uokoaji ili kumsaidia kuendelea na mchakato wa kutoa miili.

Charles Wambua
Image: HISANI

Mamia ya watu waliojitolea wamekonga nyoyo za Wakenya wengi kwa ushujaa wao wakati wa zoezi linaloendelea la kutoa miili kutoka kwa machimbo yaliyotelekezwa katika eneo la Kware, mtaa wa mabanda wa Mukuru kwa Njenga.

Charles Wambua ni mmoja wa watu waliojitolea na alikuwa mstari wa mbele kutoa miili kutoka eneo la kutupia taka. Yeye ni mfanyakazi wa kawaida katika eneo hilo na mpiga mbizi.

Hii si mara ya kwanza kwa Wambui kuhusika katika kutoa miili kutoka eneo hilo la kutupia taka.

Alisema hapo awali alihusika katika utoaji wa miili iliyotupwa katika machimbo hayo mwaka mmoja uliopita.

Kulingana na Wambua, ametoa magunia 13 yaliyokuwa na miili na sehemu za mwili katika eneo la Kware.

Wambua, akiongea na Citizen TV, alifichua kuwa mwanamke mmoja alimwendea yeye na marafiki zake na kuwafahamisha kuhusu ndoto alizokuwa nazo kuhusu dadake aliyetoweka Julai 26, 2024.

Mwanamke huyo alieleza kuwa dadake alikuwa akimuelekeza eneo la kutupia taka na ndipo walipoamua kuingia.

"Nilipozama ndani, kwanza niliutoa mwili wa msichana mdogo aliyekatwa katikati ya kiuno ili kutoshea kwenye gunia," Wambua alisema.

Alisema aliingiwa na wasiwasi na kuamua kuchunguza kilichomo kwenye magunia mengine kwenye shimo hilo lililofanana na lile la kwanza.

"Nilipotazama kwenye gunia lililofuata, niligundua mabaki ya binadamu zaidi na nilipotazama zaidi niligundua magunia mengi zaidi na yenye miili," Wambua aliongeza.

"Nilifungua kila gunia nililotoa ili kuthibitisha kilichomo."

Wambua alizitaka mamlaka husika kutoa zana muhimu za uokoaji ili kumsaidia kuendelea na mchakato wa kutoa miili kwani anaamini miili zaidi bado haijapatikana.

Idara ya Upelelezi wa Jinai ilifichua kuwa mshukiwa mkuu aliyehusishwa na mauaji hayo alikamatwa siku ya Jumatatu na kukiri kuwarubuni, kuwaua na kuwatupa wanawake 42.

Wenyeji wanatoa wito kwa serikali kutuza matendo ya ujasiri ya Wambua na wenzake.

Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja aliahidi kuwazawadia walio kazini.

"Tunawatambua na kuwapongeza vijana wa Kware waliojitolea na kuchukua uongozi katika juhudi za kuwarejesha. Tasnia yao na ushujaa wao hautapita bila malipo," Sakaja alisema kwenye taarifa.