Kenya kutuma maafisa 600 zaidi wa polisi nchini Haiti

Mataifa machache mengine kwa pamoja yameahidi takriban wanajeshi 1,900 zaidi.

Muhtasari

•Hii itafikisha kikosi cha Kenya, kilichotumwa kwa kasi tangu Juni kusaidia jeshi la polisi la taifa la Haiti kufikia 1,000.

•Hii itasababisha kuongezeka kwa fedha na rasilimali kwa ajili ya operesheni hiyo, ambayo imetatizwa na ukosefu wa vifaa.

Image: BBC

Kenya imeahidi kutuma maafisa 600 zaidi wa polisi nchini Haiti katika wiki zijazo kusaidia kupambana na magenge yanayodhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu, Port-au-Prince na maeneo ya karibu.

Hii itafikisha kikosi cha Kenya, kilichotumwa kwa kasi tangu Juni kusaidia jeshi la polisi la taifa la Haiti kufikia 1,000.

Akiwa ziarani nchini humo, Rais wa Kenya William Ruto pia alisema anaunga mkono kugeuza ujumbe wa sasa wa usalama unaoongozwa na Kenya kuwa operesheni kamili ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa.

Mataifa machache mengine kwa pamoja yameahidi takriban wanajeshi 1,900 zaidi.

Ghasia nchini Haiti bado zinaendelea na mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa magenge yanalenga maeneo mapya, na kusababisha watu wengine kuhama makazi yao.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kukutana mwishoni mwa mwezi huu ili kuamua iwapo litarejesha mamlaka ya sasa ya Kenya kwa muda wa miezi 12 zaidi, na hivyo kufungua njia kwa ujumbe kamili wa Umoja wa Mataifa mwaka 2025.

Hii itasababisha kuongezeka kwa fedha na rasilimali kwa ajili ya operesheni hiyo, ambayo imetatizwa na ukosefu wa vifaa.

Akihutubia maafisa wa polisi wa Kenya katika kituo chao cha Port-au-Prince, Rais Ruto alipongeza kikosi hicho kwa ufanisi wao katika kipindi cha miezi michache iliyopita.

"Kuna watu wengi ambao walifikiri Haiti ilikuwa misheni ambayo haiwezekani, lakini leo wamebadili mawazo yao kwa sababu ya hatua mlizopiga."

Alisema watafanikiwa dhidi ya magenge hayo na akaahidi kujaribu kuwatafutia vifaa bora.

Karibu maafisa 400 wa Kenya waliokuwa uwanjani walikuwa wakishika doria "wakishirikiana bega kwa bega na vikosi vya Haiti kulinda watu na kurejesha usalama", Ruto alisema.

"Kundi letu linalofuata, maafisa 600 wa ziada, wanaendelea na mafunzo . Tutakuwa tayari kwa misheni katika muda wa wiki chache na tunatarajia usaidizi unaohitajika ili kuwawezesha kutumwa,” aliongeza.

Lakini kumekuwa na ukosoaji fulani nchini Haiti kwa kukosekana kwa hatua madhubuti dhidi ya magenge hayo.

Mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ambaye amekuwa huko hivi punde amesema ujumbe huo haukuwa na vifaa vya kutosha na unahitaji helikopta, pamoja na miwani ya kuona usiku na ndege zisizo na rubani.

"Misheni ya Kimataifa ya Msaada wa Usalama (MSS), iliyoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mnamo Oktoba 2023, hadi sasa imetuma chini ya robo ya kikosi chake kilichopangwa," William O'Neil alisema Ijumaa .

Licha ya kuwekewa vikwazo vya kimataifa, silaha na risasi ziliendelea kuingizwa nchini kisiri na kuruhusu magenge kupanua udhibiti wao katika maeneo mapya, alisema.

Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa alikuwa ametembelea eneo la kusini-mashariki mwa nchi hiyo, ambapo alisema polisi hawana uwezo wa vifaa kukabiliana na magenge hayo.

Alimnukuu polisi mmoja huko Jérémie akisema: “Hali hiyo inapakana na mambo yasiyowezekana. Tunapaswa kujifunza kutembea juu ya maji."

Unyanyasaji wa kijinsia ulikuwa umeongezeka sana na zaidi ya watu 700,000 sasa wameyahama makazi yao, Bw O'Neil alisema.

"Uchungu huu wa kudumu lazima ukome'

Alisema suluhu tayari zipo, lakini juhudi zilipaswa "kuongezwa mara moja".

"Ni muhimu kuyazima magenge kwa kuupa Ujumbe wa MSS njia za kusaidia operesheni za Polisi wa Kitaifa wa Haiti, na pia kutekeleza hatua zingine zinazotolewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pamoja na sheria ya vikwazo vya silaha."