
ALIYEKUWA mgombea wa uenyekiti wa wadhifa wa AUC, Raila Odinga amewasuta baadhi ya wakenya ambao wamekuwa wakiibua tetesi kwamba serikali ilitumia mabilioni ya pesa katika kampeni yake.
Akizungumza katika ikulu ya Mombasa alikokaribishwa na rais
Ruto baada ya kutua nchini, wiki moja baada ya kupoteza kinyang’anyiro hicho kwa
mshindani wake kutoka Djibout, Odinga alisema kwamba ni uongo.
Mwanasiasa huyo mkongwe wa siasa za Kenya alitaja madai ya
serikali kutumia bilioni 13 kwa kampeni zake kama hekaya za Abunuwasi ambazo
hazina mashiko yoyote.
Kiongozi huyo aliwasuta wenye dhana hiyo akisema kwamba
pengine hata hawajui ‘bilioni’ ni kusema nini.
“Nimeona mabilioni
yakitajwa, watu Fulani wanasema kwamba shilingi bilioni 13 zilitumika kwa
kampeni ya Raila. Sijui ni dunia gani hao watu wanaishi na wala wanajua ni nini
bilioni inamaanisha,” Odinga alisema.
Hata hivyo, Odinga hakukanusha moja kwa moja ikiwa serikali
ilitumika pesa kwa kampeni yake au la, akisisitiza kwamba pesa ambazo
zilitumika ni zile zilihitajika tu.
“Shilingi bilioni kufanya
nini? Pesa ambazo zilitumika ni zile ambazo zilikuwa hitajika tu. Kukodisha usafiri
wa kuzunguka Afrika. Na si kwamba nilikuwa naishi maisha ghali, nilikuwa nakula
chochote ambacho kingeletwa kwangu,” alifafanua.
Odinga pia alisema kwamba kando na kutumia pesa zake, mataifa
mengi ya Afrika yalikuwa na ukarimu wa kipekee kumpa huduma kama za malazi bila
malipo.
‘Mataifa mengi ya Afrika
yalikuwa na ukarimu wa kutosha kiasi kwamba walinipa malazi na vingine vingi,
hivyo serikali ilinipa tu kile ambacho kilikuwa kinahitajika,’ alisisitiza.
Akimshukuru rais Ruto, Odinga alimrejelea kama ndugu yake
mdogo na kusema kwamba wajibu wake ulikuwa kumsaidia katika kampeni wala si
yeye aliyemsukuma kugombea.
“Ruto hakuwahi kunisukuma
niwanie. Nilijitangaza mwenyewe kwamba nilikuwa nawania uenyekiti AUC. Na yeye
[Ruto] alikuja tu kunisapoti. Na alinisapoti si tu kwa maneno bali kwa vitendo
pia,” Raila aliweka bayana.
Licha ya kampeni ya kufana iliyochukua takribani mwaka mmoja,
azma ya Raila kuliongoza bara la Afrika iliangukia pua baada ya kupoteza kwa
Mahmoud Ali Youssouf kutoka Djibout.
Youssouf alijizolea akidi stahiki ya kura 33 katika raundi ya
7 baada ya Odinga kujiondoa katika raundi ya 6 alikopata kura 22 dhidi ya 26 za
mshindi huyo.