Mwanaume apoteza maelfu ya pesa baada ya usiku wa tafrija na binti wa Mombasa

Muhtasari
  •  Mwanaume mmoja jijini Mombasa anazidi kulilia haki baada ya kupoteza pesa zinazotajwa kuwa kicha cha takriban laki sita.
  •  Mikosi yote hii ilianza baada ya mwanaume huyo kumtupia jicho la tamaa binti huyo mrembo na kisha kumuita ili wajumuike pamoja kwa kinywaji, pasi na kujua kwamba huu ndio ulikuwa mwanzo wa matatizo ya kutoweka kwa pesa zake
Image: DCI (Facebook)

Mwanaume mmoja jijini Mombasa anazidi kulilia haki baada ya kupoteza pesa zinazotajwa kuwa kicha cha takriban laki sita.

Ripoti zinasema mwanaume huyo amepoteza pesa hizo kwa njia za kutatanisha baada ya kujivinjari na binti mmoja waliyekutana jijini Mombasa.

Wawili hao walikutana kwa kile kinachotajwa kuwa usiku wa tafrija ambao baadae uligeuka kuwa mkosi kwa mwanaume baada ya kupigwa na butwaa alipogutuka na kupata ameibiwa na mwanamke huyo ambaye ametambuliwa kwa jina Wambui.

Inaripotiwa mwanamume huyoalienda Mombasa kwa safari ya kibiashara alipoamua kujivinjari katika klabu cha kifahari ambacho ni kipya huko Shanzu kwa jina la VIP Club Volume, kabla ya kukutana na kidosho huyo ambaye alimtilia “mchele” katika kinywaji chake, jambo lililompelekea mwanaume kuwa zezeta na mwanamke huyo akapata nafasi ya kumuibia pesa zake.

“Mikosi yote hii ilianza baada ya mwanaume huyo kumtupia jicho la tamaa binti huyo mrembo na kisha kumuita ili wajumuike pamoja kwa kinywaji, pasi na kujua kwamba huu ndio ulikuwa mwanzo wa matatizo ya kutoweka kwa pesa zake,” Ripoti ya DCI ilisomeka.

Wawili hao walionekana katika maongezi ya kisiri na kimahaba mno huku wakifurahia mandhari ya ukanda wa pwani na upepo mwanana wa jioni ya saa kumi, baada ya kuandamana nje na kuchukua usafiri wa teksi hadi jumba linalijulikana kama Seville Apartments, sehemu ambapo mwanaume huyo alikodi chumba kwa ajili ya mapumziko.

“Kulingana na mhasiriwa, wawili hao walikoga pamoja kabla ya kuelekea kwenye chumba cha malazi ambapo alibugia gilasi ya shabubati na pindi baada ya kumaliza akajihisi kupoteza fahamu ghafla,” ripoti hiyo ilieleza

Mwanaume huyo anasemekana kupoteza fahamu zaidi ya saa kumi na mbili mpaka kesho yake mchana wakati mhudumu katika vyumba hivyo alipobisha ili kufanya usafi wake kama kawaida na kumpata jamaa amelala yombo akiwa bado hajapata fahamu.

Mhudumu aligundua mwanaume huyu ameibiwa baada ya kupata hana vitu vyake vya muhimu kama vile simu, kipakatalishi, kadi ya ATM miongoni mwa vitu vingine alivyokuwa ameingia navyo chumbani humo.