Kenya kushirikiana na DRC na kujitenga na matamshi ya Ruto

Muhtasari

• Ubalozi wa Kenya nchini DRC umezungumzia matamshi ya Ruto kuhusu kutokuwepo kwa ng'ombe nchini humo na kuwahakikishia Wakongo kuwa mataifa haya mawili yatazidi kushirikiana kwa heshima.

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Serikali ya Kenya imejibu matamshi ya naibu rais William Ruto ambayo yalilenga kudhalilisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwamba hawana ng’ombe hata moja.

Katika taarifa iliyotolewa na balozi wa Kenya nchini Congo, George Masafu amesema kwamba  Kenya inalenga kuwa na uhusiano wa heshima na taifa la Congo.

Matamshi ya Ruto kwamba hakuna ng’ombe hata mmoja nchini DRC yalizua mtafaruku mkali kutoka kwa jamii ya wafanyabiashara na wananchi wa DRC

"Ubalozi wa Kenya ungependa kusisitiza kwamba watu wa Kenya wana ushirikiano mkubwa wa kiheshima na wa kihistoria na serikali Pamoja na wananchi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo,” alisema balozi Masafu.

"Taifa la Kenya lipo na uhakika kwamba uhusiano huu utaenezwa kupitia mifumo ya serikali moja hadi nyingine na ushirikiano baina ya wananchi, ushirikiano ambao umekuwepo tangu siku za awali,” aliendeleza kusema Masafu.