Mtoto wa Museveni hajastaafu kutoka jeshini licha ya taarifa kusema hivyo

Muhtasari

• Muhoozi Kainerugaba bado yupo jeshini na hana mpango wa kustaafu hivi karibuni hata baada ya kuandika kwenye Twitter yake kwamba amestafu hatimaye baada ya miaka 28 jeshini.

• Taarifa zilisema kwamba ni mtu anayeongoza akaunti hiyo ya Twitter alikosea kutoa taarifa hizo ambazo msemaji wa jeshi Uganda alisema ni za uongo.

KWA HISANI
KWA HISANI
Image: Muhoozi Kainerugaba

Taarifa kutoka nchini Uganda ni kwamba Luteni jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye pia ni mtoto wa rais wa muda mrefu wa nchi hiyo Yoweri Museveni, hana mipango yoyote ya kustaafu kutoka jeshini hivi karibuni licha ya taarifa za awali kuzagaa kwamba ametangaza kwenye ukurasa wake rasmi wa Twitter kustaafu baada ya kuhudumu jeshini kwa miaka 28.

Awali, Muhoozi Kainerugaba kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter alikuwa ameandika kwamba anastaafu kutoka jeshini baada ya miaka 28 ila baadae taarifa zilikua kusema kwamba ni mtu anayesimamia akaunti hiyo alikosea kwa kuandika taarifa hiyo.

Msemaji wa jeshi la Uganda Brigedia jenerali Felix Kulaigye alikanusha madai hayo na kusema kwamba Muhoozi Kainerugaba bado anaendelea kushikilia hatamu jeshini na hata hajaandika barua ya kutaka kustaafu.

Ujumbe huo kwenye Twitter ya Muhoozi ulisambaa na kuwa habari kubwa katika vyombo vya habari kote duniani lakini baadae paliibuka video ya mtoto huyo wa kwanza wa rais Museveni na Rafiki wake wa karibu mwanahabari Andrew Mwenda ambaye anasikika akimuuliza kuhusu taarifa za kustaafu ambapo Kainerugaba alizikanusha na kusisitiza kwamba kustafu ni baada ya miaka minane kamili ijayo.

Kainerugaba amekuwa akitajwa na wengi kuwa ndiye anaandaliwa ili kumrithi babake kama rais wa Uganda na wengi waliamini kwamba taarifa ya kustaafu kwake ilikuwa ni kweli na kusema kwamba ni njia moja ya kupata muda wa kutosha mbali na jeshi ili kujiweka tayari kuchukua hatamu kama rais pindi babake atakapomaliza kipindi chake cha uongozi.