Elachi: Sisi wote katika Jubilee tulichangia ongezeko la mikopo

Muhtasari

• Aliyekuwa spika wa bunge la Nairobi Beatrice Elachi amesema wote waliokuwa katika serikali ya Jubilee ndio kulaumiwa kwa ongezeko la madeni na ufisadi.

• Alisema madeni yaliongezeka katika kipindi cha kwanza cha uongozi wa Jubilee kutoka 2013-2017 ambapo pia ufisadi ulikithiri.

Katibu mkuu mwandamizi katika kitengo cha jinsia ya umma, Beatrice Elachi.
Katibu mkuu mwandamizi katika kitengo cha jinsia ya umma, Beatrice Elachi.
Image: Facebook

Aliyekuwa spika wa bunge la kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi amesema kwamba wale wanaotoroka kutoka Jubilee na kuilaumu serikali ya rais Uhuru Kenyatta kwa ongezeko la mikopo ni sharti wakubali kuwa tatizo hilo ni la kila mtu.

Akizxungumza katika kipindi cha mchana katika runinga moja nchini, Elachi alisema kwamba kila mtu ambaye alichagulia kwa tiketi ya chama cha Jubilee kutoka mwaka wa 2013, ni sharti awe tayari kulaumiwa kwa mrundiko wa mikopo ya serikali ambayo imefikia kilele sasa.

“Ndiyo, tuna deni. Nataka kuwa mwaminifu sana. Yeyote ambaye amekuwa katika serikali ya Jubilee tangu 2013 tunawajibika. Jambo hili kwamba tunakimbia matatizo tuliyoisababishia nchi yetu ni mbaya sana,” alisema Elachi.

Bila shaka wengi wamesema matamshi hayo yanamlenga naibu rais na wandani wake ambao walikigura chama cha Jubilee baada ya rais Uhuru Kenyatta kuanzisha ushirikiano na kinara wa ODM Raila Odinga, almaarufu Handshake mnamo 2018.

Elachi ambaye kwa sasa ni Katibu mkuu mwandamizi katika kitengo cha Jinsia ya umma pia aliweka wazi kwamba deni kubwa ambalo linaikumba serikali ya Jubilee lilianza kufura katika mkumbo wa kwanza wa utawala huo mwaka 2013-2017.

Pia alisema pesa nyingi za mikopo hazikufanya kazi ilivyoratibiwa kutokana na ufisadi mkubwa ambao ulikuwa unaendeshwa na baadhi ya viongozi katika serikali ya Jubilee.