Ndege ya abiria yaanguka Ziwa Victoria nchini Tanzania

Mamlaka bado haijathibitisha ni abiria wangapi walikuwa kwenye ndege hiyo na wangapi wameokolewa hadi sasa

Muhtasari
  • Askari wa zimamoto na uokoaji pamoja na polisi na wavuvi wa eneo hilo wako kwenye eneo la tukio wakifanya shughuli ya uokoaji

Ndege ya abiria imeanguka katika eneo la Ziwa Victoria mkoani Kagera.

Kamanda wa polisi mkoani humo amethibitisha kuanguka kwa ndege hiyo, na ameambia BBC kuwa uokoaji unaendelea na atatoa taarifa kwa kina baadaye.

Ndege hiyo imeanguka leo asubuhi mjini Bukoba.

Polisi wamethibitisha kutokea kwa ajali hiyo. Askari wa zimamoto na uokoaji pamoja na polisi na wavuvi wa eneo hilo wako kwenye eneo la tukio wakifanya shughuli ya uokoaji.

Mamlaka bado haijathibitisha ni abiria wangapi walikuwa kwenye ndege hiyo na wangapi wameokolewa hadi sasa, lakini kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya ndani, ndege hiyo iliyokuwa ikitokea Mwanza kuelekea Bukoba ilikuwa na abiria 49 na 23 wameokolewa hadi sasa.

BBC imezungumza na shuhuda wa tukio hilo, aliyekuwa akisubiri safari ya ndege kutoka katika uwanja wa ndege wa Bukoba.''Hapa kama dakika kumi na tano au ishirini zimepita, ndege ya Precision Air iliyokua ikitokea Dar es salaam-Mwanza- Bukoba, ilikua inakaribia kutua, nimeiona ikianguka na kuingia katika Ziwa Victoria, na naona tayari kuna zimamoto, polisi na abiria wakitijahidi kufanya uoakoaji.'' anasema Abdul Nuri.