Vipigo vya aibu kwa vilabu vikubwa vya EPL

Kipigo cha Man United na Liverpool kuathiri mbio zao za kuwania ubingwa wa EPL.

Muhtasari

•Mashetani Wekundu walipewa kipigo cha aibu na Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield siku ya Jumapili.

•Man United waliwatandika Arsenal mabao nane kwa mbili mwaka wa 2011.

Vipigo vya aibu vya vilabu vikubwa vya EPL
Image: ROSA MUMANYI

Mashetani Wekundu walipata kipigo cha aibu kwenye Uwanja wa Anfield siku ya Jumapili huku mabao saba yakipita wavuni bila wao kupata nafasi hata ya kufunga angalau bao moja la kufuta machozi.

Kipigo hicho kuliwaacha katika nafasi ya tatu wakiwa na alama 49 na kuathiri mbio zao za kuwania ubingwa wa EPL.

Washambulizi Cody Gakpo, Mohammed Salah na Darwin Nunez walifunga mabao mawili kila mmoja wakati wa mchuano huo wa kusisimua huku Mbrazil Roberto Firmino ambaye aliingia kama mchezaji wa akiba katika kipindi cha pili akifunga ushindi wa kihistoria wa Liverpool kwa bao maalum.

Ushindi wa Jumapili jioni ndio ushindi mkubwa zaidi kwa Liverpool dhidi ya Manchester United katika historia ya EPL.