Fahamu jinsi ya kulinda akaunti ya Facebook dhidi ya udukuzi

Hivi majuzi, Ukurasa wa Facebook wa Kabarak University ulidukuliwa na mwanafunzi wa Shule ya Upili wa Indonesia.

Muhtasari

•Mwanafunzi aliyedukua ukurasa wa Kabarak University alibainisha wazi kwamba alikuwa akijifurahisha tu alipofanya kitendo hicho.

•Mdukuzi alipea Kabarak University chaguo la kumlipa Ksh 68,000 ili kuwarejeshea akaunti ama kujaribu kurejesha akaunti hiyo  kama wanaweza.

Jinsi ya kulinda akaunti za Facebook.
Jinsi ya kulinda akaunti za Facebook.
Image: WILLIAM WANYOIKE.

Ukurasa wa Facebook wa Kabarak University ulioidhinishwa , wenye wafuasi zaidi ya elfu 40 ulidukuliwa siku chache zilizopita na mwanafunzi wa shule ya upili kutoka Indonesia ambaye amekuwa akichapisha vitu vyake ikiwemo picha zake.

Jumamosi, kijana huyo ambaye bado hajatambuiliwa alieleza wazi kuwa alikuwa akijifurahisha tu alipodukua akaunti hiyo na akaomba msamaha kwa hilo. Alitoa changamoto kwa taasisi hiyo  kujaribu kurejesha akaunti hiyo  kama wanaweza.

Mwanafunzi huyo wa Indonesia hata alikuwa mkarimu zaidi kupea taasisi hiyo chaguo jingine la kumlipa Ksh 68,000 ili kuwarejeshea akaunti.

Ukurasa wa Facebook wa Chuo Kikuu cha Kabarak sio wa kwanza kudukuliwa. Kila akaunti ya mtandao wowote wa kijamii iko katika hatari ya kudukuliwa haswa ikiwa hatua zifuatazo za kuzilinda hazitachukuliwa:-

  • Tunga nenosiri changamano.(complex password)
  • Tumia kidhibiti salama cha nenosiri.(secure password manager)
  • Tumia uthibitishaji wa vipengele viwili. (two-factor authentication)
  • Usishiriki maelezo ya kufungua akaunti.
  • Dhibiti majukumu ya walioidhinishwa kutumia akaunti.
  • Usibonyeze viungo (links) vya kutiliwa shaka.
  • Usikubali maombi ya urafiki ya watu usiowajua.
  • Jihadhari na barua taka na hadaa. (spam and phishing)
  • Unaposhuku umedukuliwa, wasiliana na Facebook kwa usaidizi