Fahamu ukweli kuhusu Hustler Fund

Rais William Ruto alizindua hazina ya Hustler Fund siku ya Jumanne

Muhtasari

•Wakopaji wa Hustler Fund watatumia *254# kupata mkopo huo, kampuni za mawasiliano zinazoongoza zilitangaza baada ya uzinduzi.

•Historia ya mkopo ya mkopaji pia itaamua kiasi ambacho mtu atapokea.

Fahamu ukweli Kuhusu Hustler Fund
Image: HILLARY BETT

Rais William Ruto alizindua hazina ya Hustler Fund siku ya Jumanne. Wakenya sasa wataweza kupata mikopo ya Hustler Funds kupitia simu zao za rununu.

Wakopaji wa Hustler Fund watatumia *254# kupata mkopo huo, kampuni za mawasiliano zinazoongoza zilitangaza baada ya uzinduzi.

Wakenya ambao wamejisajili kwa Safaricom, Airtel na Telekom watahitajika kubonyeza kodi hiyo fupi ili kupata mikopo. Kwa sasa, kiwango cha chini ambacho mkopaji anaweza kupata ni Ksh 500 ilihali cha juu zaidi ni na Sh50,000.

Rais  alisema wakopaji wana nafasi ya kuongeza kiwango cha mikopo yao iwapo watarejesha kabla ya siku ya mwisho ya kurejesha iliyotolewa.

Waziri wa Vyama vya Ushirika na Maendeleo ya SMEs Simon Chelugui alisema viwango vya mikopo vitaongezeka kulingana na tabia ya mkopaji.

"Kiwango kitapitiwa upya na kurekebishwa kulingana na historia ya ukopaji na urejeshaji wa mikopo ya awali iliyochukuliwa," alisema.

Historia ya mkopo ya mkopaji pia itaamua kiasi ambacho mtu atapokea.

 Chelugui alisema hakutakuwa na usajili unaohitajika kwa Huster Fund. Alisema wakopaji watatumia kodi fupi ya SMS ambayo itawaelekeza kwenye menyu fulani, ambayo itawongoza hadi kwenye usajili wa mkopo.

Waziri aliongeza kuwa wafanyikazi watahitaji tu simu zao, kwani hakutakuwa na mawakala wa mchakato huo.Aidha, alitangaza kuanzishwa kwa kituo cha simu ambacho kitajibu maswala na maswali ya wakopaji.