Trump Mashakani

Maseneta wa Marekani wapiga kura kuendelea na mashtaka dhidi ya Trump

Iwapo atapatikana na hatia Bw Trump anaweza kukabiliwa na kuzuiwa kugombe urais tena

Muhtasari
  • Bw Trump anashutumiwa kwa "kuchochea uasi" wakati kikao cha Congress kilipovamiwa mwezi uliopita.
  • Mawakili watetezi wa Trump walidai kuwa hawezi kukabiliwa na kesi baada ya kuondoka Ikulu ya White House.

 

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump

 Bunge la Seneti la Marekani limebaini kuwa kesi ya mashitaka dhidi ya rais wa zamani Donald Trump ni ya kikatiba, na hivyo kuruhusu mchakato mzima wa kesi kuanza.

Mawakili watetezi wa Trump walidai kuwa hawezi kukabiliwa na kesi baada ya kuondoka Ikulu ya White House.

Lakini Maseneta 56 walipiga kura ya kutaka kesi hiyo iendelee huku 44 wakipiga kura ya kupinga , huku baadhi ya wabunge wachache wa chama cha Republican wakiunga mkono hatua hiyo.

 

Bw Trump anashutumiwa kwa "kuchochea uasi" wakati kikao cha Congress kilipovamiwa mwezi uliopita.

Maelfu ya watu walikusanyika kuunga mkono madai ya uongo kwamba kulikuwa na wizi wa kura katika maeneo mengi ambao ulimnyima ushindi Bw Trump katikauchaguzi wa urais.

Waendesha mashitaka wa upande wa chama cha Democrats walifungua mchakato wa Jumanne wa kwa mashitaka kwa kuonesha video ya hotuba aliyoitoa Bw Trump tarehe 6 Januari na maandamano ya ghasia yaliyofanywa na baadhi ya wafuasi wake.

"Huo ni uhalifu wa hali ya juu wa upotovu ," Mbunge Jamie Raskin wa Maryland alisema katika video hiyo "Kama hilo sio kosa la kushitakiwa , basi hakuna kitu kama hicho ."

Mawakili wa rais huyo wa zamani walidai kuwa ni kinyume cha katiba kumuweka rais wa zamani katika mchakato kabisa na wakawashutumu Democrats kwa kuchochewa kisiasa.

Kwa idadi ya waliopigia kura kuendelea kwa kesi 56 na 44 waliopinga, inamaanisha kuwa Warepublicans sita waliunga mkono kuendelea kwa kesi dhidi ya Trump.

Ingawa hii inaonesha kuwa baadhi wa hawana mafungamano na chama chochote cha kisiasa , matokeo haya yanaonesha bado kuna ufuasi mkubwa wa rais wa zamani katika chama chake.

 

Theluthi mbili ya wabunge inahitajika ili kuidhinisha kesi hiyo dhidi ya Trump katika bunge lla Seneti lenye wabunge 100 lenye mgawanyiko mkubwa.

Iwapo atapatikana na hatia Bw Trump anaweza kukabiliwa na kuzuiwa kugombe urais tena

Nini kilichotokea Jumanne ?

Kesi ilianza kwa mameneja wa mashitaka- Wademocrats waliopewa jukumu la kuongoza mashitaka-wakidai mchakato wao wa kumshitaka Trump ulikuwa na halali kisheria.

Katika video ya dakika 10 iliyotumiwa katika ufunguzi wa mchakato huo, Bw Trump alionyeshwa akiwaambia wafuasi wake ku "wapigane wawezavyo " kabla ya kuvamia jengo la Congress la marekani- Capitol katika ghasia zilizosababisha vifo vya watu watano - ikiwa ni pamoja na afisa wa polisi.

Rep Raskin alilia kwa machozi alipolkuwa akielezea hofu ya usalama wa familia yake wakati wa ghasia hizo wakati alipotenganishwa na binti yake aliyekuja kumtembelea.

" Hii haiwezi kuwa hali ya baadae ya Marekani," aliwaambia maseneta, ambao walikuwa kama wazee wa mahakama kwa ajili ya mashitaka hayo.

"Hatuwezi kuwa na maraisi wanaochochea na kuhamasisha magenge ya ghasia dhidi ya serikali yetu na taasisi kwasababu wamekataa kukubali utashi wa watu chiniya katiba ya Marekani ."

Mawakili wa Bw Trump walionesha msimamo wao wa kuainisha hoja zao zilizojaa malalamishi na madai kuuhusu mchakato na uhalaki wa kikatiba wa mchakato wa kumshitaki mteja wao.

Mwendesha mashitaka wa zamani wa Pennsylvania Bruce Castor alinza utetezi wa Bw Trump kwa maelezo marefu ambayo yalipingwa hata na washirika wa Bw Trump.

Wakili wa pili, David Schoen, alikuwa bayana zaidi. Alionesha kikao viodeo kuanzia mwaka 2017 kama ushahidi wa kile alichokitaja kama "ukosefu wa sababu tosha ya mashitaka " miongoni mwa wabunge wa Democratic .

Sasa kila upande una hadi saa 16 kuwasilisha hoja yao kuanzia saa sita mchana Jumatano.

Hoja hizi zinatarajiwa kuendelea kutolewa hadi mwishoni mwa juma wakati maseneta wa pande zote watapata fursa ya kutoa hoja zao.

Haijawa wazi ikiwa mameneja wa mashitaka wataongeza muda wa ratiba ya maswali na majibu na kuomba mashahidi waitwe au warekodiwe ushahidi wao - licha ya kwamba Bw trump tayari amekwisha kataa kujitolea kutoa ushahidi.

Wabunge wa pande zote wanasemekana kuwa wanataka kesi iwe ya haraka, huku juhudi zikiendelea za kumtaka Rais Joe Biden aidhinishe fedha za msaada wa virusi vya corona.

Kwa ratiba ya haraka, inadhaniwa kuwa kura ya Seneti kuhusu kumtia hatiani au kumuondolea mashitaka Bw Trump kufikia Jumatatu.