Mzozo wa Tigray Ethiopia: Ripoti yasema uhalifu wa kivita huenda ulifanyika

Muhtasari
  • Mauaji ya kiholela, mateso, ubakaji na mashambulizi dhidi ya wakimbizi na watu waliohama makwao yote yametajwa
Image: BBC

Pande zote kwenye mzozo wa jimbo la Tigray nchini Ethiopia zimekiuka haki za kibinadamu, ukiukaji unaoweza kutajwa kuwa uhalifu dhidi ya binadamu, kwa mujibu wa ripoti mpya.

Mauaji ya kiholela, mateso, ubakaji na mashambulizi dhidi ya wakimbizi na watu waliohama makwao yote yametajwa.

Uchunguzi wa pamoja uliofanya na tume ya haki za binadamu nchini Ethiopia na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ulisema kuwa pia huenda kuna ushahidi wa uhalifu wa kivita.

Vita vilizuka Novemba 4 mwaka 2020

Vilianza wakati waziri mkuu wa Ethiopia Abiy aliamrisha uvamizi dhidi ya vikosi vya jimbo la kaskazini mwa nchi la Tigray.

Wanajeshi wa serikali wakati huo waliwatimua waasi lakini mambo yalibadilika mwezi Juni wakati wapiganaji wa Tigray walipata mafanikio. Kwa sasa wanaripotiwa kukaribia mji mkuu, Addis Ababa.

Siku ya Jumanne serikali ya Ethiopia ilitangaza hali ya hatari saa chache baada ya kutoa wito kwa wakaazi wa mji mkuu kujihami.

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet, anasema mzozo huo umekumbwa na ukatili mbaya na kutoa wito wa kusitishwa mapigano.

"Kuna sababu za kutosha kuamini kuwa pande zote katika mzozo moja kwa moja zilishambulia raia, au mali ya raia, kama nyumba, shule, hospitali na maeneo ya kuabudia au kufanya mashambulizi yaliyosababisha vifo vya raia na kuharibu mali ya raia," ripoti hiyo ilisema.

Mauaji ya kiholela pia nayo yameripotiwa

Ripoti hiyo inaeleza jinsi vijana kutoka Tigray wanaofahamika kama Samri waliwaua watu 200 kutoka jamii ya Amhara eneo la Mai Kadra mwezi Novemba mwaka uliopita.

Mauaji ya kilipiza kisasi kisha yakaendeshwa dhidi ya jamii ya Tigrinya katika mji huo huo.

Jeshi la Eritrea limejiunga kwenye mzozo huo likiwasaidia wanajeshi wa serikali ya Ethiopia. Wanajeshi wa Eritrea waliwaua zaidi ya raia 100 eneo la Axum kati kati mwa Tigray mwezi Novemba mwaka 2020, kulinga na ripoti hiyo.

'Uhalifu wa kivita huenda umetekelezwa kwa kuwa kuna sababu na kwa kuwa watu ambao hawakushiriki kwenye ukatili waliuawa na wale walioshiriki katika mzozo," ripoti inasema.

Ripoti hiyo pia inasema kuwa kuna kesi za ukatili wa kingono ukiwemo ubakaji na kutoa wito kwa serikali ya Ethiopia kufanya uchunguzi kwa kutumia mashirika huru kuhusu madai ya ukiukaji wa haki na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika.

Waziri mkuu Abiy alisema kwamba aliagiza mashambulizi ya kijeshi mwezi Novemba ili kujibu shambulizi dhidi ya kambi moja iliokuwa na wanajeshi wa serikali.

Mzozo huo unajiri baada ya mgogoro wa miezi kadhaa kati ya serikiali ya Abiy na viongozi wa TPLF , ambacho ndio chama kinachotawala jimbo la Tigray.

Mamlaka baadaye ilitaja kundi la TPLF kuwa shirika la kigaidi na kukataa mazungumzo yoyote ya amani nalo.

Serikali iliimarisha mashambulizi ya ardhini katika wiki za hivi karibuni ,pamoja na yale ya angani dhidi ya kundi hilo lakini haikufanikiwa kuwazuia wapiganaji hao wanaoendelea kuteka maeneo kadhaa.

Katika taarifa siku ya Jumatano, bwana Abiy alisema kwamba serikali yake ilikuwa na wasiwasi mwingi kuhusu ripoti hiyo ya pamoja lakini akaongezea kwamba serikali yake iliumizwa na kwanini uchunguzi huo haukufichua madai ya mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Tigray na haikutoa ushahidi wowote kwamba serikali iliwanyima kimakusudi misaada ya kibinadamu raia wa jimbo la Tigray.

Msemaji wa chama cha TPLF alisema kwamba ripoti hiyo ina makosa mengi , akisema kwamba kushirikishwa kwa EHRC ndio chanzo cha kukosekana kwa usawa .