Covid- 19: Ufaransa yasema Omicron inasambaa kwa kasi ya radi

Muhtasari

•Ulaya tayari imeshuhudia visa zaidi ya milioni 89 na vifo vya watu milioni 1.5 vinavyohusiana na Covid, kulingana na takwimu za hivi karibu za EU.

•Kulikuwa na misururu mirefu ya magari katika Port of Dover Ijuamaa huku watu wakijaribu kuingia Ufaransa kabla ya kuanza utekelezwaji wa masharti ya kusafiri Jumamosi

Image: REUTERS

Aina ya Corona ya Omicron "inasambaa kwa kasi ya radi'' katika Ulaya na huenda ikawa ndio watu wengi watakayougua zaidi nchini Ufaransa kufikia mwanzoni mwa mwaka ujao , Waziri mkuu wa Ufaransa Jean Castex ametahadharisha..

Alizungumza Ijumaa, saa chache kabla ya Ufaransa kuweka masharti ya kusafiri kwa wale wanaoingia nchini humo kutoka Uingereza.

Kufikia sasa Uingereza ndio nchi iliyoathiriwa zaidi miongoni mwa mataifa ya Ulaya, huku karibu watu 15, 000 wakithibitshwa kupata maambukizi ya kirusi kipya cha Omicron Ijumaa.

Katika maeneo yote ya bara hilo, maafisa wa afya wanakabiliana na wimbi la maambukizi.

Masharti zaidi ya kuzuwia kusambaa kwa virusi hivyo yalitangazwa na Ujerumani, Jamuhuri ya Ireland na Uholanzi Ijumaa huku serikali zikitaka kumaliza maambukizi,.

Ulaya tayari imeshuhudia visa zaidi ya milioni 89 na vifo vya watu milioni 1.5 vinavyohusiana na Covid, kulingana na takwimu za hivi karibu za EU.

Lakini waziri wa afya wa Ujerumani Karl Lauterbach aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa kuwa nchi "lazima ijiandae kwa changamoto ambayo hatujawahi kuwa nayo kwa muundo huu", huku shirika lake la afya ya umma ikizitaja Ufaransa, Norway, na Denmark kama ''maeneo hatari'' kutokana na kuogezeka kwa maambukizi katika nchi hizo.

Ujerumani yenyewe iliripoti zaidi ya visa 42,000 vya maambukizi Jumamosi, vikiwa ni chini ya visa vipya 50,000 vya maambukizi vilivyorekodiwa Ijumaa.

Ireland, ambako theluthi ya visa vipya vimetokana na omicron, Taoiseach Micheál Martin alisema kuwa wanatarajia "kushuhudia maambukizi kwa kiwango ambacho ni zaidi ya kile ambacho kimewahi kushuhudiwa hadi sasa".

Tahadhari hiyo inakuja huku Uingereza ikiripoti idadi ya maambukizi kwa siku ya tatu- hadi watu 93,000- wengi wao wakiwa na maambukizi ya kirusi kipya cha Omicron.

Ufaransa ilifunga mipaka yake kwa watu wanaosafiri kutoka Uingereza kwa shuguli za biashara na utalii saa tano usiku Ijumaa, huku misururu mirefu ya watu ikishuhudiwa katika maeneo ya kuabiri ndege ya Port of Dover na Eurostar huku watu wakijarubu kuingia kabla ya marufuku ya safari kuanza kutekelezwa.

Sio nchi pekee iliyoweka mashari makali zaidi ya kudhibiti corona. Mapema wiki hii , Italia, Ugiriki na Ureno zilitangaza kuwa wageni wote kutoka Muungano wa EU watahitaji kuwasilisha matokeo hasi ya covid wanapowasili-hata wale ambao wamechanjwa.

Akizungumza saa chache kabla ya sheria pya kuwekwa, Bw Castex alisema masharti ya kusafiri ni sehemu ya msururu wa hatua zilizoletwa ili kuzuia maambukizi. .

Hatua hizo ni pamoja na kupunguza muda baina ya dozi ya pili nay a tatu ya chanjo, na itahitaji mtu kuwa amechanjwa ili kuweza kuingia katika mgahawa au hoteli na kusafiri mwendo mrefu katika usafiri wa umma.

Zaidi ya hayo, sherehe zote rasmi za kumaliza mwaka na ufyatuaji wa fataki vimeahirishwa.

Image: REUTERS

Kulikuwa na misururu mirefu ya magari katika Port of Dover Ijuamaa huku watu wakijaribu kuingia Ufaransa kabla ya kuanza utekelezwaji wa masharti ya kusafiri Jumamosi

Wakat huo huo, nchini Uholanzi, Wataalamu wa afya wamesema kuwa nchi inatakiwa kuingia katika kipindi cha ''masharti makali'' ya lockdown, vimeripoti vyombo vya habari nchini humo.

Waziri mkuu Mark Rutte amesema Omicron inaweza kuwa kirusi kilichosambaa zaidi nchini humo mwezi Januari, sawa ana Ufaransa.

Uholanzi ilirekodi visa zaidi ya 15,400 vya maambukizi Ijumaa-vikiwa ni chini ya vile vilivyorekodiwa siku zilizopita, lakini vikiwa ni vya juu zaidi kuliko vilivyowahi kutangazwa wakati wa janga.

Bwana Castex pia amesema kuwa serikali itatangaza hatua mpya za kushugulikia wanaosita kuchanjwa, akisema "haikubaliki kwamba kukataa kwa Wafaransa milioni chache kuchanjwa kuliweke taifa zima hatarini''