Binti wa mwanadiplomasia akatwa kichwa kwa kukataa kuolewa

Muhtasari
  • Picha za CCTV zilimuonesha akijaribu kutoroka bila mafanikio
  • Mauaji hayo yalizua taharuki nchini kote na kusababisha madai ya kutaka jitihada zaidi kufanywa ili kuhakikisha usalama wa wanawake unakuepo

Mahakama nchini Pakistani imemuhukumu adhabu ya kifo mwanaume mmoja kwa kosa la kumbaka na kumuua binti wa mwanadiplomasia wa zamani, ambaye alikataa ombi lake la kuolewa.

Noor Muqaddam, aliyekuwa na umri wa miaka 27, alipigwa, kubakwa na kukatwa kichwa na Zahir Jaffer, ambaye ni mtoto wa miongoni mwa familia tajiri zaidi nchini Pakistan.

Mauaji hayo ya kikatili yalifanyika nyumbani kwake tarehe 20 Julai mwaka jana. Picha za CCTV zilimuonesha akijaribu kutoroka bila mafanikio.

Mauaji hayo yalizua taharuki nchini kote na kusababisha madai ya kutaka jitihada zaidi kufanywa ili kuhakikisha usalama wa wanawake unakuepo.

Mauaji ya Noor Muqaddam na mwanaume aliyemfahamu katika kundi moja la marafiki wa jamii ya kiitajiri yalikuwa yametawala vichwa vya habari kwa miezi kadhaa.

Ilileta wito wa kufanyiwa marekebisho mfumo wa haki ya jinai wa Pakistan, ambao una viwango vya chini sana vya hatia, hasa kwa uhalifu dhidi ya wanawake.

Mamia ya wanawake huuawa nchini humo kila mwaka, na maelfu huteswa huku kesi nyingi zikiwa haziripotiwi.

'Maelezo ya kuinua nywele yametolewa mahakamani'

Baada ya kifo chake, wengi walidai haki kwa Noor. Familia yake ilikuwepo katika mahakama iliyojaa watu mjini Islamabad na walikuwa na hisia kali wakati hakimu akiposoma uamuzi huo.

Jaffer alimteka Noor Muqaddam kwa muda wa siku mbili katika nyumba ya familia yake katika wilaya ya kifahari ya mji mkuu baada ya kukataa kuolewa naye.

Katika kusikiliza kesi hiyo Jaffer aliwaambia waandishi wa habari kuwa aliuwa akiwa nje ya mahakama akizungukwa na polisi : "Nilikuwa na hasira, nilimuua Noor kwa kisu."

Maelezo ya kuinua nywele yaliyoshirikiwa katika mahakama yalishtua Pakistan. Wanaharakati wa haki za wanawake waliingia mitaani na kulikuwa na mishumaa.

Wanawake wengi walijitokeza na kushiriki hadithi zao za unyanyasaji wa nyumbani na unyanyasaji wa kijinsia.

Wafanyikazi wawili wa nyumbani kwa Jaffer walihukumiwa kifungo cha miaka 10 kwa kusaidia mauaji hayo, huku wazazi wake waliachiliwa kwa kujaribu kuficha ukweli wa kilichotokea.

Baba yake, Shaukat Muqaddam, alisema uamuzi huo kuwa ni ushindi wa haki na akasema anataka kuhakikisha wanyanyasaji na wauaji wa wanawake nchini Pakistani hawakimbii uhalifu wao tena.

"Nina furaha kwamba haki imetendeka," alisema.

"Nimekuwa nikisema kwamba hii sio kesi ya binti yangu tu, ni kesi ya mabinti wote wa nchi yangu."

Aliahidi kupinga kuachiliwa kwa wazazi wa Jaffer.

Jaffer, mwenye umri wa miaka 30 raia wa Marekani mwenye asili ya Pakistani, pia anaweza kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.