Mchungaji akamatwa kwa kosa la usafirishaji haramu wa binadamu Tanzania

Image: MFALME ZUMARIDI/INSTAGRAM

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia Diana Bundala maarufu kama "Mfalme Zumaridi kwa kosa la usafirishaji haramu wa binadamu vilevile unyonyaji wa kujipatia kipato.

Tarehe 26 mwezi Februari,jeshi la polisi mkoa wa Mwanza lilimkamata mtu huyo ambaye ni mchungaji wa kanisa.

''Alikamatwa kwa kosa la usafirishaji wa watu 149, mtakumbuka juzi tarehe 23 polisi jijini mwanza walipokea amri ya mahakama ya kwenda kumkamata mtoto aitwaye Samir Ally Abas aliyetakiwa kufikishwa kwenye mahakama ya mwanzo kwa kosa la kutokwenda shule baada ya mtoto kutoroshwa na mama yake, baada ya msako ilibainika mama na mtoto wamehifadhiwa katika nyumba ya 'mfalme Zumaridi', alisema kamanda wa mkoa wa Mwanza Ramadhani Ng'anzi

Kamanda amesema walipofika eneo hilo walimtafuta mmiliki wa makazi hayo, na kumtaka amsalimishe mzazi wa mtoto huyo lakini alikataa alikataa kufanya hivyo. Polisi waliamua kumkamata mchungaji huyo.

Kamanda huyo wa polisi amesema kuwa walibaini ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na watu zaidi ya 149 waliokuwa wanaishi pale hivyo polisi walimkamata kiongozi huyo wa kanisa kwa ajili ya mahojiano.

Pia walibaini kuwepo kwa watoto wa umri kati ya miaka 4 mpaka kumi na saba, ambao wamekuwa wakifungiwa hapo kwa muda mrefu.

''Mkiangalia umri huo wa miaka 4-17 ni umri ambao watoto hao wanapaswa kuwa katika madarasa mbalimbali wakipata elimu na tulipowahoji wazazi wao walipo watoto hao hawakueleza vizuri wazazi wao walipo.''

Uchunguzi unafanyika kubaini kwanini mwanamke huyu anawashikilia watu wengi nyumbani kwake na mkusanyiko mkubwa wakifanya ibada bila kibali wakifanya ibada nyumbani kwake.

Atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika, akishutumiwa kuwazuia askari kufanya kazi yao , lakini pia kuwashikilia watu wengi wakiwemo watoto bila uhalali.