Akaunti ya Twitter ya Jenerali Muhoozi Kainerugaba, 'mrithi' na mwanawe rais Museveni yatoweka

Muhtasari

• Akaunti ya Twitter ya Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mwanawe Yoweri Museveni imepotea miezi michache baada ya kuingua Urusi mkono katika mzozo wa Ukraine.

KWA HISANI
KWA HISANI
Image: Muhoozi Kainerugaba

Akaunti ya Twitter ya Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mwanawe rais wa Uganda Yoweri Museveni umetoweka Jumanne kwa njia isiyojulikana.

Bado haijabainika wazi kama akaunti hiyo ilifutiliwa mbali na mamlaka ya mtandao huo wa Twitter wenyewe ama na Muhoozi aliamua kuifuta.

Lakini wajuzi wa masuala ya mitandaoni wanasema akaunti hiyo huenda ilifungwa tu na Muhoozi kwani inapotafutwa kwa kuandika jina lake inakuambia kwa sasa haipo kumaanisha kwamba imefungwa.

Mwanawe huyo wa rais Museveni kwa muda mrefu amekuwa akitajwa kuwa anaendelea kuandaliwa na uongozi wa babake ili kuwa mrithi wake pindi atakapoamua kuachia madaraka kama rais wa taifa hilo.

Kando na kuwa ndiye mrithi mtarajiwa wa babake, Muhoozi alikabidhiwa cheo kikubwa katika jeshi la Uganda kama njia moja ya kumuandaa kuwa rais baada ya babake.

Wiki kadhaa zilizopita wakati Urusi iliivamia Ukraine, Muhoozi aligonga vichwa vya habari baada ya kutangaza wazi kwamba anaiunga mkono Urusi kwa hatua hiyo ya kuishambulia Ukraine, jambo lilioonekana kuenda kinyume na mataifa mengi ya Magharibi ambayo yalikuwa mstari wa mbele kukashfu uvamizi huo.

Pia aliibua mjadala kwenye Twitter alipotangaza kwamba baada ya kuhudumu kwenye jeshi la Uganda kwa miaka 28, hatimaye amestaafu jeshini na kujiunga uraiani, madai ambayo siku moja baadaye aliyafutilia mbali na kusema kwamba mtu anayemsaidia kuendesha shughuli za akaunti hiyo yake ndiye alikosea kutoa taarifa hiyo.