"Big Boys!"Rais wa Rwanda Paul Kagame kuhudhuria 'birthday' ya mtoto wa Museveni, Muhoozi Kainerugaba

Chilling with the Big Boys

Muhtasari

• Rais wa Rwanda Paul kagame anatarajiwa kuhudhuria hafla ya siku ya kuzaliwa ya mwanawe rais Yoweri Museveni wa Uganda.

• Hafla hiyo ya kusherehekea miaka 48 ya kuzaliwa kwa Muhoozi Kainerugaba itafanyika tarehe 23 na 24 kwenye Ikulu ya Uganda

KWA HISANI
KWA HISANI
Image: Muhoozi Kainerugaba

Mwanawe rais Yoweri Museveni, Muhoozi Kainerugaba ametoa orodha ya watu mashuhuri ambao watahudhuria hafla ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa ya kufikisha umri wa miaka 48.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Kainerugaba amekuwa akitaja watu mbali mbali huku akisema watakuwepo katika hafla hiyo ambayo itafanyika kama hafla ya kitaifa vile, lakini ni kusherehekea siku yake ya kuzaliwa tu!

Miongoni mwa watu mashuhuri ambao wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo ya Kainerugaba ni pamoja na rais wa muda mrefu wa nchi Jirani ya Rwanda Paul Kagame.

“Nina furaha sana kutangaza kwamba mjomba wangu, Kamanda mkuu, Rais na Kiongozi wa Rwanda atahudhuria sherehe yangu ya kuzaliwa. Ruhanga asiimwe! Inkotanyi cane kweli,” aliandika Muhoozi kwenye Twitter yake

Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika tarehe 23 mwezi huu wa Aprili katika ukumbi wa Lugogo Cricket Oval ambapo itaendelea mpaka tarehe 24 Aprili wakati chakula cha jioni kitaandaliwa katika ikulu ya Kampala na rais Museveni mwenyewe.

Hafla hiyo ambayo imesisitizwa kuwa itahudhuriwa na watu waalikwa pekee pia itawaona mastaa wa muziki kama Bebe Cool na Jose Chameleone wakitumbuiza.

Muhoozi Kainerugaba ambaye ni jenerali mkuu wa majeshi ya Uganda, UPDF amekuwa akipigiwa upato na vibaraka wa uongozi wa Museveni kuwa ndiye chaguo bora anayezidi kukuzwa ili kuchukua nafasi ya urais wa taifa hilo la Afrika Mashariki pindi babake ‘atakapochoka’ na uongozi.