Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan apigwa risasi na kujeruhiwa kwenye maandamano

Msaidizi mkuu aliliambia shirika la habari la AFP: "Hili lilikuwa jaribio la kumuua’

Muhtasari
  • Bw Khan, 70, alikuwa akiongoza maandamano kuelekea  mji mkuu Islamabad kudai uchaguzi wa haraka

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Imran Khan amepigwa risasi na kujeruhiwa wakati wa maandamano katika mji wa mashariki wa Lahore, katika jaribio linaloonekana kuwa la mauaji.

Wanachama wa chama chake cha PTI walisema watu wengine wanne walijeruhiwa siku ya Alhamisi - lakini hakuna aliyeuawa.

Haijabainika iwapo alipigwa mguu au wayo, lakini msaidizi alinukuliwa akisema hakuwa hatarini.

Bw Khan, 70, alikuwa akiongoza maandamano kuelekea  mji mkuu Islamabad kudai uchaguzi wa haraka.

Msaidizi mkuu aliliambia shirika la habari la AFP: "Hili lilikuwa jaribio la kumuua’

Mshukiwa wa kiume alikamatwa baadaye, kulingana na Geo TV ya Pakistani.

Mwezi uliopita, tume ya uchaguzi ya Pakistani ilimnyima Bw Khan kushikilia wadhifa wa umma katika kesi iliyoelezwa na mchezaji huyo nyota wa zamani kuwa ilichochewa kisiasa.

Alikuwa ameshutumiwa kwa kutangaza kimakosa maelezo ya zawadi kutoka kwa wakuu wa kigeni na mapato kutokana na madai ya mauzo yao. Zawadi hizo ni pamoja na saa za Rolex, pete na viunganishi vya mikono ya shati