Donald Trump kuwania tena urais wa Marekani

Ni nadra sana rais wa zamani wa Marekani kutaka kutwaa tena uongozi baada ya kushindwa.

Muhtasari

•Trump alizindua nia yake hiyo - ya tatu ya urais - siku ya Jumanne katika eneo lake la Mar-a-Lago huko Florida.

Image: BBC

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ametangaza nia yake ya kugombea tena Urais na kurudi Ikulu ya White House mnamo 2024.

Trump alizindua nia yake hiyo - ya tatu ya urais - siku ya Jumanne katika eneo lake la Mar-a-Lago huko Florida, wiki moja baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula ambapo Republican walishindwa kushinda viti vingi katika Congress kama walivyotarajia.

Ni jaribio nadra sana la kiongozi wa zamani wa Marekani kutaka kutwaa tena Ikulu ya White House baada ya kushindwa katika uchaguzi.

Katika hotuba iliyotangazwa moja kwa moja na televisheni ya Marekani, Trump alizungumza na mamia ya wafuasi wake kwenye ukumbi uliopambwa kwa vinara kadhaa na kupambwa na bendera nyingi za Marekani.

"Ili kuifanya Amerika kuwa bora tena, leo usiku natangaza nia yangu ya kuwa rais wa Marekani," Trump alisema kwa umati wa wafadhili na wafuasi wa muda mrefu waliokuwa wakipunga simu.

"Ninagombea kwa sababu ninaamini ulimwengu bado haujaona utukufu wa kweli wa kile taifa hili linaweza kuwa," alisema. "Tutaweka tena Amerika kwanza," aliongeza.

Donald Trump anapozungumza huko Mar-a-Lago, wafuasi wanapokea simu za michango katika vikasha vyao vya barua pepe.