Kiongozi mstaafu wa kanisa Katoliki, Papa Benedict 16 ameaga dunia na miaka 95

Siku mbili zilizopita, mrithi wake Papa Francis alitoa wito kwa Ulimwengu kumuombea mkongwe huyo, katika kile alitaja kuwa alikuwa "anaumwa sana"

Muhtasari

• Benedict alijiuzulu mwaka 2013 kama Papa na amekuwa akiishi katika himaya  ya Watakatifu ya Vatican.

• Alikuwa mtakatifu wa kwanza kufanya uamuzi wa kuachia ngazi mamlaka kama Papa kwa zaidi ya miaka 600 iliyopita.

• Katika saa chache zijazo, Holy See Press Office itawasilisha maelezo ya ibada ya mazishi.

Papa Benedict 16
Papa Benedict 16
Image: BBC News

Ulimwengu unaomboleza kifo cha Papa Benedict wa 16 aliyeaga asubuhi ya Jumamosi Desemba 31 akiwa na umri wa miaka 95.

The Holy See Press Office ilitangaza kwamba Papa Emeritus alikufa saa 9:34 asubuhi Jumamosi asubuhi katika makazi yake katika Monasteri ya Mater Ecclesiae, ambayo Papa huyo mstaafu mwenye umri wa miaka 95 alichagua kama makazi yake baada ya kujiuzulu kutoka kwa huduma ya Petrine mnamo 2013.

“Kwa masikitiko ninawajulisha kwamba Papa Mstaafu, Benedict XVI, amefariki dunia leo saa 9:34 asubuhi katika Monasteri ya Mater Ecclesiae mjini Vatican. Taarifa zaidi zitatolewa haraka iwezekanavyo. Kuanzia Jumatatu asubuhi, tarehe 2 Januari 2023, mwili wa Papa Mstaafu utakuwa katika Basilica ya Mtakatifu Petro ili waumini waweze kuaga."

Taarifa hizi zinakuja siku mbili tu baada ya papa Francis ambaye ni mrithi wake kutoa taarifa kwa umma akiwataka watu kumuweka Papa huyo mkongwe kwenye maombi na sala maalum katika kile alitaja kuwa “alikuwa anaumwa sana”

Katika saa chache zijazo, Holy See Press Office itawasilisha maelezo ya ibada ya mazishi.

Benedict aliwashangaza waumini wa Kikatoliki na wataalamu wa kidini kote ulimwenguni Februari 11, 2013, alipotangaza mipango ya kujiuzulu wadhifa wake wa Papa, akitaja "umri wake mkubwa."

Katika hotuba yake ya kuaga, papa anayemaliza muda wake aliahidi kukaa "mafichoni" kutoka kwa ulimwengu, lakini aliendelea kuzungumza juu ya mambo ya kidini katika miaka iliyofuata baada ya kustaafu, na kuchangia mvutano ndani ya Kanisa Katoliki.

Alikuwa mtakatifu wa kwanza kufanya uamuzi wa kuachia ngazi mamlaka kama Papa kwa zaidi ya miaka 600 iliyopita.

Kinyume na Benedicto wa 16 ambaye alikuwa na misimamo mikali dhidi ya mapenzi ya jinsia moja, mrithi wake Papa Francisco katika miaka ya hivi karibuni amekuwa akinukuliwa kwa njia mbalimbali akionekana kukaribisha suala la mapenzi ya jinsia moja katika kanisa.

Alizaliwa kwa jina Joseph Ratzinger  nchini Ujerumani mwaka wa 1927, alikuwa mtoto wa polisi. Alitawazwa kuwa padre mwaka wa 1951, akawa kardinali mwaka wa 1977, na baadaye akahudumu kama mshauri mkuu wa kitheolojia wa Papa Yohane Paulo II.

Alichaguliwa kuwa papa mnamo Aprili 2005, kufuatia kifo cha John Paul II.

Alijulikana kuwa na msimamo mkali zaidi kuliko mrithi wake, Papa Francis, ambaye alichukua hatua za kupunguza msimamo wa Vatican juu ya uavyaji mimba na ushoga, pamoja na kufanya zaidi kukabiliana na janga la unyanyasaji wa kijinsia ambalo limelikumba kanisa hilo katika miaka ya hivi karibuni na kugunduliwa.