Museveni: Kumuadhibu mke katika ndoa si hatia, ni jambo la kawaida kitamaduni

Museveni alilinganisha kumchapa mke kama kumchapa mwizi pindi anapopatikana akifanya wizi.

Muhtasari

• Nchini Kenya, visa vya kuadhibu mke kwa viboko au watoto shuleni ni hatia ambayo inaweza kukuzolea kifungo jela.

rais Museveni na mkewe Janet
rais Museveni na mkewe Janet
Image: Maktaba

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amezua gumzo pevu mitandaoni baada ya kudai kuwa katika tamaduni za Kiafrika, si vibaya mwanaume kumuadhibu mke wake kwa kumtwanga viboko.

Katika video moja ambayo imesambazwa mitandaoni, rais Museveni alikuwa anazungumza kuwa mke kuadhibiwa na mumewe ni sawa tu na jinsi mwizi anaadhibiwa na umati wa watu wengi pindi anapopatikana akitekeleza uhalifu.

Rais huyo mkongwe alisema kuwa tamaduni za Kiafrika zinaruhusu hilo, ila si kwa kuadhibu mke hadi kumuumiza au kumuua.

“Katika tamaduni za Kiafrika, kumcharaza mwizi ni kitu halali. Ni kama Saudi Arabia ambapo mtu akikamatwa anafanya usherati anafaa kuuawa au kupigwa mawe. Katika jamii ndio maana kuna adhabu ya wengi kutokana kwa watu, sio mimi. Mwizi anauawa na watu kama polisi hayuko karibu. Sio tu kumchapa mwizi ndio halali, bali pia hata kumchapa mke wao kitamaduni ni sawa. Pia watoto kuwaadhibu ni halali kama wamekosea,” Museveni alisema katika video hiyo ambayo haijulikani ni ya lini.

Ushauri huu wa Museveni unakinzana na kile ambacho makundi ya kupigana vita dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia yanahubiri.

Nchini Kenya, visa vya kuadhibu mkeo katika ndoa kwa kumtia vibao ni hatia kubwa huku pia adhabu ya viboko kwa watoto shuleni ikipigwa marufuku miaka michache iliyopita.

Maneno hayo ya kuhalalisha adhabu ya viboko katika ndoa kutoka kwa rais wa Uganda si mageni kwani wengi wanajua na kuelewa jinsi kiongozi huyo anavyoendesha Uganda ambapo kwa mara kadhaa mrengo wa upinzani umekuwa ukimtuhumu kwa kuongoza nchi Kidhalimu.