Mwanamume akamatwa akiuza misalaba 22 aliyoiba kutoka kwa makaburi

Mwanamume huyo alikamatwa katika duka la kuuza vyumba kuukuu akijaribu kunadi misalaba hiyo wakati aliitiwa polisi.

Muhtasari

• Mshukiwa huyo atafikishwa mahakamani hivi karibuni kujibu kesi ya uvamizi wa makaburi na kuzua usumbufu kwa marehemu.

Misalaba iliyoibwa kutoka kwa makaburi
Misalaba iliyoibwa kutoka kwa makaburi
Image: Malawi24

Ukistaajabu ya Musa ya Fimbo yake basi hujayaona ya Firauni na pembe zake ndefu!

Nchini Malawi, mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 42 alizua kioja baada ya kuelekea makaburini na kung’oa misalaba yote kwenye makaburi ya watu waliozikwa kitambo na hivi karibuni.

Lengo lake?

Inaarifiwa kuwa kijana huyo aliyetambulika kwa jina Mapeto Kanyama alikuwa na njaa ya pesa na wakati ameketi chini ya kivuli cha mti na uvivu wake, wazo lilimjia, likamtuma katika makaburi ya Kijiji kilichoitwa cha Robert eneo la Mchinji.

Akaamua kuvamia makaburi yapatao 22 na kung’oa misalaba iliyokuwa imetundikwa kama ishara na dhibitisho kuwa marehemu walizikwa hapo huku majina yao yakiwa yameandikwa kwenye misalaba hiyo pamoja na tarehe za kuzaliwa, na kufa.

Msemaji wa polisi wa Mchinji, Limbani Mpinganjira, aliambia chombo cha habari cha Malawi 24 kuwa polisi walimkamata Kanyama baada ya kumkuta akiwa na misalaba.

Kanyama alilitiwa mbaroni katika duka la kupima uzani wa vyuma kuukuu na kuviuza.

Kulingana na kituo hicho cha habari, Mshukiwa huyo atafikishwa mahakamani hivi karibuni kujibu kesi ya uvamizi wa makaburi na kuzua usumbufu kwa marehemu.

Taarifa ilisema kuwa ombi lilitumwa kwa jamaa za marehemu wote kujitokeza katika kituo cha polisi anakoshikiliwa mshukiwa huyo ili kutambua misalaba ya makabauri ya wapendwa ndugu zao waliotanguliwa mbele za haki.

Hatari hii mzee!