Tundu Lissu arejea Tanzania baada ya miaka mitano nje ya nchi

Lissu alieleza kuwa ili kutatua changamoto hiyo ya kupanda kwa gharama za maisha ni vyema wananchi wakaungana kusaka katiba mpya

Muhtasari
  • Kiongozi wa Upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema ugumu wa maisha unaowakabili watanzania ni tatizo la kimsingi linalosababishwa na mambo ya kibinadamu na ya kisiasa

Baada ya takribani miaka mitano nje ya nchi, hatimaye mwanasiasa wa upinzani, Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki na mwanasheria nguli, aliyepata kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Antiphas Lissu, amewasili nchini Tanzania siku ya leo.

Tundu Lissu alianza kuishi uhamishoni nchini Ubelgiji baada ya kuondoka Kenya, Januari 2018 alipokuwa akipatiwa matibabu. Ni baada ya kunusurika shambulio la mauaji Septemba 7, 2017, katikati mwa Tanzania, Dodoma. Shambulio lililomuacha na matundu 16 ya risasi.

Bw Lissu alipokelewa na wafuasi wake waliokuja kumlaki, ambapo alipata fursa ya kuongea nao:

Kiongozi wa Upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema ugumu wa maisha unaowakabili watanzania ni tatizo la kimsingi linalosababishwa na mambo ya kibinadamu na ya kisiasa.

"Kwa sababu ni mambo ya kisiasa tuna mamlaka ya kuyaondoa, kwa hiyo kama umechoka na kushindwa kununua maharage, sembe au tozo, hili liko ndani ya uwezo wetu, halihitaji maombi wala kumtwisha Mungu mambo yaliyopo kwenye uwezo wetu," amesema Lissu muda mfupi baada ya kurejea nchini Tanzania leo akitokea uhamishoni.

Lissu alieleza kuwa ili kutatua changamoto hiyo ya kupanda kwa gharama za maisha ni vyema wananchi wakaungana kusaka katiba mpya ili iwe suluhu ya changamoto.Kiongozi huyo ambaye aliishi uhamishoni kwa takribani miaka mitano, alisema licha ya kutokuwa na uwezo kimamlaka wa kushughulika upandaji wa gharama nchini Tanzania lakini hatoacha kulizungumzia.

"Nataka nijitetee kwamba mimi sina mamlaka kisheria ya kupunguza bei hiyo, sina isipokuwa kuyazungumza tu...hiyo nitaifanya haihitaji niwe na kacheo fulani," alisema Lissu ambaye pia alikuwa Mgombea urais nchini katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

KATIBA MPYA

Lissu ameeleza kuwa iwapo Katiba mpya itapatikana italeta suluhu kwenye changamoto nyingi zinazoikabili nchi ikiwemo upandaji wa gharama za maisha.

Lissu alisema, "Kwa wale wenye Katiba kuna kamstari mahali kwenye Katiba, kanakoelezea kwanini bei ya maharage ni sawa na bei ya nyama, Katiba inampa mamlaka makubwa Rais wa kuamua watu watozwe nini na kwa wakati gani.”