Gavana wa Taliban auawa katika ofisi yake

Gavana wa jimbo la Balkh kaskazini mwa Afghanistan ameuawa katika shambulio la kujitoa mhanga.

Muhtasari

• Ndiye afisa mkuu wa Taliban kuuawa tangu wanamgambo hao warejee mamlakani mwaka 2021.

Gavana wa Taliban Muzamili aliuawa katika ofisi yake
Gavana wa Taliban Muzamili aliuawa katika ofisi yake
Image: Taliban

Gavana wa Taliban wa jimbo la Balkh kaskazini mwa Afghanistan ameuawa katika shambulio la kujitoa mhanga linalodaiwa na kundi la Islamic State (IS).

Mohammad Dawood Muzammil aliuawa katika ofisi yake katika mji mkuu wa mkoa, wa Mazar-e Sharif, siku ya Alhamisi.

Ndiye afisa mkuu wa Taliban kuuawa tangu wanamgambo hao warejee mamlakani mwaka 2021.

Ghasia zimepungua sana tangu wakati huo, lakini maafisa wakuu wanaounga mkono kundi la taliban wamekuwa wakilengwa na IS.

Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid alisema kwenye Twitter kwamba gavana huyo "aliuawa kama shahidi katika mlipuko wa maadui wa Uislamu".

Muzammil alikuwa ameongoza vita dhidi ya IS katika wadhifa wake wa awali kama gavana wa jimbo la mashariki la Nangarhar. Alihamishiwa Balkh Oktoba iliyopita.

Msemaji wa polisi wa Balkh Mohammed Asif Waziri alisema mlipuko huo ulitokea Alhamisi asubuhi kwenye ghorofa ya pili ya ofisi ya gavana.

"Kulikuwa na kishindo. Nilianguka chini," Khairuddin, ambaye alijeruhiwa katika mlipuko huo, aliliambia shirika la habari la AFP. Alisema ameona rafiki yake akipoteza mkono katika mlipuko huo.